Suala la
baadhi ya Watanzania kuhifadhi mabilioni ya fedha nchini Uswisi
limechukua sura mpya, baada ya tume maalumu kuwahoji vigogo 200 wakiwamo
wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Habari
zilizopatikana zinaeleza kuwa tume hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema tayari imeshafanya kazi hiyo kwa
miezi miwili sasa.
Tume hiyo
maalumu iliyoundwa na Serikali kwa Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni
mwa mwaka jana, inatarajiwa kukamilisha uchunguzi huo wakati wowote
kuanzia sasa na kuwasilisha ripoti hiyo katika kikao kijacho cha Bunge.
Jaji Werema alipoulizwa na Mwananchi Jumpili maendeleo ya uchunguzi huo,
alisema kuwa kazi hiyo bado inaendelea.
“Uchunguzi
huo unaendelea,” alisema Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya
kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa
sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Mwanasheria huyo wa Serikali alikataa kutaja baadhi ya majina ya watu ambao tume yake imewahoji mpaka sasa.
Alisema
anashangazwa na swali la namna hiyo, kwa maelezo kwamba ni jambo ambalo
liko wazi kuwa ni kinyume na maadili kuwataja watuhumiwa wakati huu
uchunguzi ukiwa bado unaendelea.
Uchunguzi
huo unafanyika baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa
mwezi Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki
nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la
kimataifa la uchunguzi la The Indian Ocean Newsletter toleo la hivi
karibuni, lilimnukuu Werema akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia
matumaini.
Werema
anaripotiwa akiri kuwa uchunguzi huo umefikia ‘hatua ya kutia matumaini’
na wanaendelea na kazi hiyo kwa uangalifu ili kuwa na uhakika wa
taarifa wanazozitafuta.
Alisema
kwamba taarifa ya awali inatarajiwa kutolewa hivi karibuni na tayari
idadi kubwa ya wahusika wakiwamo wabunge wameshahojiwa.
Werema alisema wanaendelea na uchunguzi kuwabaini zaidi ya Watanzania 200, waliotajwa kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Mbali na
Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama vile
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk
Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa
Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Tume hiyo
inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa
kutoka idara ya upelelezi na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
Serikali.
Kwa mujibu
wa jarida hilo la kimataifa, miongoni mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na
majenerali wastaafu wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya Dola 133 milioni
mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya
watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia
zao, akaunti zao za benki zilizoko nchini na nje ya nchi pamoja na nchi
walizotembelea mara kwa mara kwa miaka mitatu iliyopita.
Lengo la
kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa
katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa
huko zilipatikana kihalali.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa Bungeni kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Bunge
liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia Oktoba mwaka
huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.



No comments:
Post a Comment