Wabunge  watano wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliofukuzwa  bungeni wiki iliyopita na kupewa adhabu ya siku tano ya kutohudhuria  vikao vya Bunge la bajeti, wameanza kukusanya orodha ya wananchi katika  mikoa minne, wakiomba ridhaa yao kuunga mkono hoja binafsi  itakayowasilishwa bungeni baada ya Aprili 30, mwaka huu.
Hoja hiyo  inalitaka Bunge liilazimishe serikali kupunguza athari za ongezeko la  kupaa kwa gharama za maisha na kudhibiti mfumuko wa bei.
Mbunge wa  jimbo la Ubungo, John Mnyika, ambaye ameungana na wabunge hao katika  ziara hiyo maalumu ya kukishitaki kiti cha Spika wa Bunge, Anna Makinda  na Naibu wake, Job Ndugai, alisema Chadema inakusanya sahihi za wananchi  katika mikoa ya Iringa, Njombe, Dodoma na Mbeya ili kupata ridhaa ya  umma itakayotimiza matakwa ya kikanuni kwa mujibu wa sheria za Bunge.
Mnyika  alikuwa alitangaza dhamira hiyo jana wakati akihutubia mkutano wa  hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa,  Manispaa ya Iringa muda mfupi  kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Willibrod Slaa,  kuzungumzia madai ya Chadema kuhusishwa na vitendo vya ugaidi. “Wananchi  wangu naomba mjiandikishe kwenye hizo karatasi zinazopita huko kwenu na  kuweka sahihi zenu kwa sababu tunataka ridhaa ya umma inayopendekeza  Bunge liisimamie (liilazimishe) serikali ipunguze athari za ongezeko la  gharama za maisha kwa wananchi na kudhibiti mfumuko wa bei nchini…Hakuna  anayependa kuona anakosa makazi, sukari inapanda bei, chakula bei juu  halafu serikali hii hii inakaa kimya,” alisema Mnyika.
Kwa mujibu  wa Mbunge huyo hoja yake ambayo amedai kuwa ataiwasilisha bungeni baada  ya Aprili 30 mwaka huu, inatokana na kanuni ya 34 ya kanuni za kudumu za  Bunge.
Hadi mkutano huo unaahirishwa jana jioni, zaidi ya watu 300 walikuwa wamejiorodhesha kukubaliana na hoja hiyo.
Dk. Slaa  alisema licha ya Chama chake kuhusishwa na propaganda chafu za masuala  ya ugaidi, yeye mwenyewe yupo tayari kutekwa, kuteswa, kuuawa na hata  kungolewa macho na meno, lakini hatoacha kuzungumzia mambo yanayohusu  maslahi mustakabali wa taifa.
“Nilitaja  mafisadi 11 pale Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, lakini hadi leo  sijakamatwa wala kesi kufunguliwa, kwa maana hiyo kama nilikuwa nimesema  uongo leo hii ungekuta ninaoezea jela. Lazima wajue (CCM na serikali  yake) kwamba Chadema hatuogopi kwa sababu tulianza na Mungu na  tutamaliza na Mungu na kwa maana hiyo niko tayari kutekwa, kuteswa,  kung’olewa macho, kucha na kuuawa, lakini si kuzibwa mdomo nisizungumzie  mustakabali wa nchi,”  alisema.
Aliwaagiza   wabunge wote wa Chadema kuhakikisha kuwa kila hotuba ya Mawaziri vivuli  wa chama hicho na michango yote ya wabunge wake itakayosomwa bungeni  hivi sasa wanaidurufu na kuisambaza kwenye kila kata na ngazi zote za  vijiji ili wananchi wajue nini viongozi wao wanachokifanya ndani ya  bunge hilo.
Hata  hivyo,hali ya usalama katika uwanja huo jana ilionekana kuimarika zaidi  kutokana na makachero wa Polisi kutanda kila kona huku Dk. Slaa  akiimarishiwa ulinzi kwa askari waliovaa sare kandokando ya jukwaa kuu.
Wakati huo  huo, Dk. Slaa leo anaongoza timu ya wabunge tisa wa Chama hicho katika  mkutano wa hadhara unaofanyika jijini Mbeya wenye lengo la kuwaeleza  wananchi sababu za baadhi ya wabunge wa Chadema kufukuzwa bungeni.
Katibu  Mwenezi wa Chadema wilaya ya Mbeya Mjini, Christopher Mwamsiku, alisema  ugeni huo mkubwa unaingia Mbeya kwa lengo moja kubwa la kukijenga chama  na kutoa ufafanuzi wa kina wa sababu za kufukuzwa bungeni kwa wabunge  wao, akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la  Mr. II Sugu.
“Wageni wetu  tunawapokea kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya  Ruandanzovwe, mkutano ambao utaongozwa na Katibu wa Chadema Taifa, Dk.  Slaa.
CHANZO: NIPASHE



No comments:
Post a Comment