MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa (CHADEMA), amehoji ni lini serikali itarekebisha mwonekano
ulioanza kujitokeza kwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kutoa
habari kwa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kwa kuwa wakati wa uongozi wa Tido
Mhando TBC ilionekana kama ndege ambayo inapaa na kuwafanya Watanzania
wengi kujenga imani na chombo hicho kwa maana ya kupata habari za
uhakika na zisizo na upendeleo…
“Lakini kwa sasa shirika limekuwa kama
ndege ambayo inarudi chini kutokana na kushindwa kutoa habari kama
ilivyokuwa awali na sasa imekuwa ikitangaza habari za upendeleo wa
kukibeba chama tawala (CCM). Je, serikali ina kauli gani kwa wananchi
kuwa sasa wataanza kujenga imani na chombo hicho ambacho kimeishaanza
kupoteza imani kwa wananchi?” alihoji mchungaji Msigwa.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti
Maalumu, Amina Abdulla Amour (CUF) alitaka kujua ni mikoa mingapi
inakosa matangazo ya TBC hadi sasa.
Aidha, alitaka kuelewa serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha shirika hilo linasikika kwa kurusha matangazo yake nchi nzima.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amoss Makala, alisema si kweli
shirika hilo linatangaza habari zake kwa kukipendelea Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Makala alisema mikoa ambayo haipati
matangazo ya redio ni tisa ambayo ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja,
Mjini Magharibi, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Geita, Mtwara, Njombe na
Simiyu.
SOURCE: Chadema Social Media