Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By | Blog Gadgets Via Blogger Widgets

Thursday, June 13, 2013

BAJETI KUSOMWA LEO


WAKATI bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 inatarajiwa kusomwa leo bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, wananchi wanaingojea kwa shauku kubwa kuona kama itawapa ahueni ya maisha.
Tayari mwelekeo wa bajeti hiyo unaonyesha kuwa watumiaji wa simu za mkononi sasa watalazimika kuumia zaidi baada ya Bunge kupendekeza kuanzishwa kodi mpya ya kadi za simu za mkononi (Sim-Card).
Kodi hiyo ambayo ni moja ya vyanzo vipya vilivyoanishwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, inatarajiwa kukusanya sh bilioni 255. 5 kwa mwaka.
Wakati Watanzania wakisubiri maumivu hayo, serikali imetumia kiasi cha sh trilioni 1.8 kugharimia magari yake ya kifahari, maarufu kama ‘mashangingi’ kwa miaka mitatu tu, ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2012/13 iliyotengewa sh trilioni 1.2.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) anayeongoza Kamati ya Bunge ya Bajeti, alisema kamati yake imeainisha maeneo mapya 24 ambayo kama yatafanyiwa kazi, yataliingizia taifa zaidi ya sh trilioni 3.9 kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Eneo lingine lililoainishwa na kamati hiyo ni pamoja na kuanzisha kodi mpya katika huduma za usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi ambapo itaiingizia serikali kiasi cha sh bilioni 25.5.
Wanywaji wa vileo, wavuta sigara watarajie maumivu zaidi katika bidhaa hizo kwani ni dhahiri kwamba serikali itaendelea kuongeza kodi.
Maeneo mengine yaliyoainishwa na kamati hiyo ambayo yanaweza kuongeza pato la kodi ya ndani au kupunguza gharama za matumizi, ni umeme, bandari, viwanja vya ndege, reli, uvuvi, viwanda, misitu, na utalii.
Kamati hiyo iliainisha eneo la utumiaji wa makaa ya mawe na gesi badala ya mafuta kwamba likitumika vizuri, linaweza kuokoa sh trilioni 1.1 ambazo kwa sasa serikali inatumia kuzalisha umeme.
Iliainisha kuwa mauzo ya gesi baada ya bomba la gesi la Mtwara kukamilika, yataiingizia serikali kiasi cha sh bilioni 129.02 kwa mwaka 2015, na sh bilioni 353.62 kwa mwaka 2017.
Kuhusu hasara inayopata serikali kutokana na ununuzi wa magari makubwa na ya anasa usiozingatia gharama za uendeshaji, Chenge alisema kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, gharama za mafuta, mafunzo na matengenezo, zimeligharimu taifa sh trilioni 1.8.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, mapato ya serikali yanayotarajiwa kukusanywa ni kiasi cha sh trilioni 10.6 Serikali Kuu, sh trilioni 9.9 ni mapato ya Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na sh bilioni 741 ni mapato yasiyo ya kodi, sh bilioni 372 halmashauri na sh trilioni 3.8 ni fedha za nje.
Kipaumbele cha pili cha serikali katika bajeti hiyo ni kuboresha miundombinu ya bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo.
Vipaumbele vingine ni reli, maji, elimu, sekta za afya, ujasiriamali na kilimo.
Kabla ya kusomwa kwa bajeti hiyo ambayo itasomwa muda mmoja kwa mataifa yote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira atawasilisha bungeni mwelekeo wa uchumi kwa mwaka huu wa 2012/2013 na ujuo wa 2013/2014.
Matarajio ya wananchi ni kuona Kamati ya Chenge imefanikiwa kuibua vyanzo vipya vya mapato kwenye sekta kubwa kama madini na utalii badala ya kutegemea vinywaji vikali, baridi na sigara.
Pia kuondolewa ama kupungua kwa kodi na ushuru kwenye pembejeo na zana za kilimo kutatoa unafuu kwa wakulima kujiongezea kipato na kuzalisha kwa wingi.
Kiu ya wananchi wengi hususani wafanyakazi, itakuwa kwenye ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa siku ya maadhimisho ya Mei Mosi kuwa serikali itapunguza kodi kwenye mishahara pamoja na kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma.
Pia wafanyabiashara wakubwa watapenda kusikia kama watapata unafuu wa kodi ya mapato, huku wadogo ambao mapato yao ni ya chini wakitaraji kuondolewa kodi.
Katika mwaka huu wa fedha, serikali imepanga kutumia sh trilioni 18.5 huku ikiweka kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya umeme.
Bajeti hiyo ilitanguliwa na bajeti za wizara za serikali, ambapo kulitokea msuguano mkali kwa wabunge wakishinikiza bajeti za Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi kuongezwa.
Pamoja na matrilioni ya shilingi yanayotengwa kwenye bajeti za wizara hizo, kamati za Bunge zimebaini fedha hizo kutotolewa zote na serikali hatua inayokwamisha utekelezaji wa majukumu ya wizara mbalimbali.

Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...