MHESHIMIWA OMAR YUSSUF MZEE |
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
kuwa Baraza lako tukufu likae kama Kamati maalum ya kujadili na hatimae
kuidhinisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka 2013/14. Ombi
hili linalenga kutimiza matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
kama ilivyorekebishwa. Kama ilivyo desturi, sambamba na Hotuba hii,
naomba pia kuwasilisha Mapitio ya Hali ya Uchumi mwaka 2012 na
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka 2012/13 kama
yanavyoonekana katika Kitabu cha Kwanza. Aidha, katika Kitabu cha Pili
nawasilisha Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka
2013/14 na mwisho ni rasimu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2013/14. Naomba maelezo hayo nayo yawekwe katika kumbukumbu za Baraza.
2. Mheshimiwa Spika, tumekutana tena
hapa kuzungumzia Mipango muhimu ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake,
Wazanzibari. Naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba kwa kutubariki
uwezo huu wa kujumuika tena leo hii. Namuomba atujaalie hekima katika
kukiendesha kikao hiki muhimu na tumalize kikao tukiwa tumewatumikia
vyema, kwa busara na kwa ukweli Wananchi wenzetu tunaowawakilisha.
3. Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia
kipindi chengine cha juhudi kubwa kwa Mheshimiwa Rais wetu na wasaidizi
wake katika kutuletea maendeleo. Tumeshuhudia pia kuimarika kwa amani na
utulivu nchini petu, pamoja na matukio machache yaliyoashiria kuharibu
utulivu wetu. Hatua za haraka za kuyadhibiti matukio hayo
zilizochukuliwa na Serikali yetu zimeweza kurejesha hali ya nchi kuwa ya
shwari. Kifungu cha 26 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinatamka
kwamba Rais ndie “Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya
Mapinduzi, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi”. Hatua za maendeleo na
utulivu tunazozishuhudia, kwa hivyo, ni matokeo ya uongozi huo wa
Mheshimiwa Rais. Naomba basi nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza
sana Mheshimiwa Dr. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake uliojaa hekima, busara na kuona
mbali. Kwangu binafsi, namshukuru pia kwa kuendelea kuniamini na kunipa
jukumu la kuiongoza Ofisi yake hii muhimu inayoshughulikia Fedha, Uchumi
na Mipango ya Maendeleo.
4. Mheshimiwa Spika, nimesema kuwa
tulikuwa na matukio machache ya kuharibu utulivu katika kipindi hiki.
Miongoni mwa matukio hayo ya kusikitisha na kutia huzuni ni yale ya
kushambuliwa na kuathiriwa kwa viongozi tofauti wa dini na Sheha.
Kwanza, Sheikh Fadhil Soraga, aliemwagiwa tindikali mapema ya asubuhi ya
tarehe 6 Novemba 2012. Likafuatia tukio la kupigwa risasi kwa Mchungaji
Amros Mkenda asubuhi ya tarehe 25 Disemba mwaka 2012. Mwenyezi Mungu
muumba alituonesha uwezo wake, akamlinda na kwa rehema zake bado Padri
Mkenda yuko hai. Tukio kubwa zaidi ni lile lililotokea asubuhi ya tarehe
17 Februari mwaka huu kwa kupigwa risasi na kuuwawa kwa Mchungaji
Everest Mushi. Tukio la karibuni kabisa ni la kumwagiwa tindikali Sheha
wa Shehia ya Tomondo, Bw. Mohammed Said Kidevu lililotokea tarehe 23 Mei
mwaka huu.
5. Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile
matukio yote hayo yalilenga kuwadhuru kwa kiasi kikubwa viongozi wetu
hao wa dini zetu kubwa na shehia; yalilenga kuleta fitna kubwa katika
jamii yetu kwa kugombanisha waumini wa dini tofauti; na hatimae
yalilenga kuleta fujo nchini na kuondoa utulivu uliozoeleka.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuepusha na shari zote za matukio hayo
na kutuepusha na makusudio ya wahusika. Nawashukuru na kuwapongeza sana
wananchi wote, na hasa ndugu, jamaa na wafuasi wa karibu wa viongozi
wote hao. Nawashukuru na kuwapongeza kwa utulivu wao na imani yao kwa
Serikali katika kipindi chote cha majaribu.
6. Mheshimiwa Spika, wakati Serikali
bado inaendelea na jitihada za kuwapeleka wahusika katika mikono ya
sheria, tuendelee wote kunasihiana katika kudumisha utulivu tuliouonesha
wakati wachache wetu walipotutia majaribuni. Kwa Sheikh Soraga,
Mchungaji Mkenda na Sheha Mohammed Kidevu tunawaombea kwa Muumba muweza
awaponyeshe haraka na kuwaondolea khofu ya matukio yao. Kwa Mchungaji
Mushi tunamuombea malazi mema na kwa ndugu, marafiki na waumini wake
tunawaombea subira zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu atalipa kwao kwa subira
yao na hataacha kuwalipa waliotenda uovu huu kwa dhulma yao kwa viongozi
hao wote wasio na hatia.
7. Mheshimiwa Spika, naamini uongozi
mzuri wa Mheshimiwa Rais umesaidiwa pia na utendaji na ushauri anaoupata
kutoka kwa wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad,
Makamo wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa
Pili wa Rais. Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati Makamo hao
wa Rais kwa uongozi wao.
8. Mheshimiwa Spika, kipindi kama hiki
mwaka jana, wananchi wenzetu wa Jimbo la Bububu hawakuwa na Mwakilishi
katika Baraza hili kufuatia kifo cha aliekuwa Mwakilishi wao, Salum
Amour Mtondoo. Kupitia uchaguzi mdogo, tayari pengo hilo limezibwa, na
limezibwa vyema. Nawapongeza sana wananchi wa Jimbo la Bububu kwa
kuchagua Muwakilishi wao. Na mimi nachukua fursa hii kumpongeza sana
Mheshimiwa Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa) kwa kuchaguliwa kuliwakilisha
Jimbo hilo humu Barazani. Naamini kwa utendaji aliouonesha Mheshimiwa
Hussein tokea kuchaguliwa kwake, wananchi hao wameridhika na chaguo lao.
Namtakia kila la kheri Mheshimiwa Hussein katika kuwatumikia na
kuwawakilisha vyema wananchi wa Jimbo la Bububu.
9. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi
huo, naomba sasa niwasilishe Mapitio ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2012
na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka 2012/13 hadi
kufikia Machi 2013.
MAPITIO YA UCHUMI NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI KWA MWAKA 2012/13
Hali ya Uchumi Duniani na Kikanda
10. Mheshimiwa Spika, uchumi wa dunia
unaendelea kukua taratibu kutokana na matatizo ya kiuchumi na fedha
yaliozikumba nchi za Ulaya. Uchumi wa dunia mwaka 2012 umekuwa kwa
wastani wa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia
4.0 mwaka 2011. Kanda zote nazo zimeshuhudia kasi ndogo ya kukua kwa
uchumi wake kwa mwaka 2012, kama hivi ifuatavyo:
(i) Uchumi wa nchi zilizoendelea umekuwa kwa wastani wa asilimia 1.2 kutoka asilimia 1.6 mwaka 2011;
(ii) Uchumi wa nchi zinazoendelea na zinazoibuka kiuchumi umekuwa kwa wastani wa asilimia 5.1 kutoka asilimia 6.4 mwaka 2011;
(iii) Uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara umekua kwa wastani wa asilimia 4.8 kutoka asilimia 5.3 mwaka 2011; na
(iv) Katika Afrika ya Mashariki ukuaji ulifikia wastani wa asilimia 4.5 kutoka asilima 5.9 mwaka 2011.
MFUMKO WA BEI WA DUNIA, AFRIKA NA KANDA
11. Mheshimiwa Spika, tofauti na ukuaji
wa uchumi, mwenendo wa utulivu wa bei za bidhaa na huduma Duniani na
katika Kanda zote umekuwa wa kuridhisha kwa mwaka 2012, kwa kupungua
kasi ya wastani wa mfumko wa bei, kama inavyobainishwa hapa chini:
(i) Kasi ya mfumko wa bei duniani imepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2011 kufikia 3.3 mwaka 2012;
(ii) Kwa nchi zilizoendelea ilishuka na kufikia asilimia 1.3 mwaka 2012 kutoka asilimia 1.4 mwaka 2011;
(iii) Kwa nchi zinazoibuka kiuchumi na
zinazoendelea ilishuka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2011 na kufikia
asilimia 5.9 mwaka 2012; na
(iv) Nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la
Sahara mfumko wa bei ulipungua hadi asilimia 9.1 mwaka 2012 kutoka
asilimia 9.3 mwaka 2011.
(v) Kwa nchi za Afrika ya Mashariki, ulishuka kutoka asilimia 13.2 mwaka 2011 hadi wastani wa asilimia 11.5 mwaka 2012.
MWENENDO WA UCHUMI WA ZANZIBAR
Pato la Taifa
12. Mheshimiwa Spika, uchumi wa Zanzibar
umeonesha mwenendo mzuri tofauti na ule wa dunia na Kanda. Ukuaji
halisi wa uchumi umeimarika zaidi mwaka 2012 na kufikia asilimia 7.0
ikilinganishwa na asilimia 6.7 wa mwaka 2011. Pato la Taifa kwa bei za
miaka husika limefikia jumla ya TZS 1,354 bilioni mwaka 2012
ikilinganishwa na TZS 1,198 bilioni kwa mwaka 2011.
Miongoni mwa mambo yaliyochangia ukuaji huo ni pamoja na haya yafuatayo:
(i) Ongezeko la ukuzaji rasilimali kwa
asilimia 41.3 kutoka thamani ya TZS 183.20 bilioni mwaka 2011 mpaka TZS
258.87 bilioni. Ongezeko hili limesababishwa na uwekezaji mkubwa katika
maeneo ya ujenzi wa nyumba za kuishi na biashara, zana za usafirishaji
na ujenzi vijijini.
(ii) Ukuaji mzuri wa sekta ya viwanda ambayo imekua kwa asilimia 9.2 mwaka 2012 kutoka asilimia 5.8 mwaka 2011.
(iii) Kuimarika kwa sekta ya huduma ambayo imekuwa kwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.6 mwaka 2011.
PATO LA MTU BINAFSI
13. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
kiasi hicho cha Pato la Taifa na idadi ya watu milioni moja na laki tatu
wa Zanzibar, kwa wastani, Pato la kila mtu limeongezeka mwaka 2012 na
kufikia TZS 1,003,000/= (USD 638) kwa mwaka kutoka TZS 960,000/= (USD
617) mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 4.5.
UKUAJI NA MICHANGO YA KISEKTA KATIKA PATO LA TAIFA
14. Mheshimiwa Spika, kiujumla, sekta
zote zimeonesha ukuaji katika mwaka 2012 ingawa kwa viwango tofauti na
kwa kasi tofauti ikilinganishwa na mwaka 2011. Viwango hivyo vya ukuaji
kwa mwaka 2012 ni kama hivi ifuatavyo:
(i) Sekta ya Huduma ilikuwa kwa asilimia 8.7 ikionesha kuimarika kidogo kutoka asilimia 8.6 mwaka 2011;
(ii) Sekta ya Kilimo ilikuwa kwa asilimia 1.3 na hivyo kasi yake imeshuka kutoka asilimia 2.7 ya mwaka 2011; na
(iii) Ukuaji wa Sekta ya Viwanda
ulifikia asilimia 9.2 kutoka asilimia 5.8 ya mwaka 2011, ukichangiwa
zaidi na kuimarika kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za kuishi na za
biashara.
15. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
mchango ya Sekta hizi katika Pato la Taifa, mchango wa Sekta ya Huduma
umeimarika zaidi na kufikia asilimia 45.3 kutoka asilimia 44.0 mwaka
2011. Matokeo ya kuimarika huko ni kushusha michango ya sekta nyengine.
Sekta ya Kilimo imechangia asilimia 30.2 kutoka asilimia 32.2 mwaka 2011
wakati sekta ya Viwanda imechangia asilimia 11.7 mwaka 2012 kutoka
mchango wa asilimia 12.0 mwaka 2011.
MFUMKO WA BEI ZANZIBAR
16. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa bei
Zanzibar umeshabihiana na ule wa dunia na Kanda kwa mwaka 2012. Kasi ya
mfumko wa bei ilipungua hadi kufikia asilimia 9.4 na hivyo kuwa juu
kidogo kuliko matarajio ya kufikia asilimia 8.7. Hata hivyo, bado kasi
hii ni chini ya kiwango cha wastani wa nchi za Afrika ya Mashariki.
Kufikiwa kiwango cha tarakimu moja ni hatua nzuri ikilinganishwa na
kiwango cha Mfumko wa Bei cha asilimia 14.7 kwa mwaka 2011. Kwa kuwa
sehemu kubwa ya Mfumko wa Bei Zanzibar inachangiwa na uingizaji bidhaa,
kasi nafuu ya Mfumko wa Bei imechangiwa na utulivu wa bei katika nchi
tunazofanya nazo biashara, mwenendo mzuri wa bei za chakula na mafuta ya
Petroli katika soko la dunia na utulivu wa thamani ya sarafu ya
Tanzania kulinganisha na Dola ya Marekani.
SEKTA YA NJE
17. Mheshimiwa Spika, Mizania ya
Biashara inaonesha kuwa nakisi katika urari wa biashara imeendelea
kupanuka zaidi mwaka 2012 na kufikia TZS 203.9 bilioni kutoka nakisi ya
TZS 102.9 bilioni ya mwaka 2011. Hali hii imechangiwa na kasi kubwa ya
kukua kwa uingizaji ikilinganishwa na ukuaji wa usafirishaji bidhaa nje.
Katika mwaka huo, uingizaji ulikuwa kwa asilimia 65.2 kutoka TZS 164.2
bilioni mwaka 2011 hadi TZS 271.3 bilioni mwaka 2012. Kwa upande
mwengine, katika kipindi hicho usafirishaji ulikuwa kwa asilimia 10 tu
kutoka TZS 61.3 bilioni hadi TZS 67.4 bilioni. Hali hii imetokana na
kasi kubwa zaidi ya uingizaji wa vifaa vya chuma kama nondo, mashine na
vifaa vya umeme.
UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI 2012/13
18. Mheshimiwa Spika, Baraza lako
liliidhinisha Bajeti ya TZS 648.9 bilioni kwa mwaka wa fedha 2012/13,
zikihusisha TZS 315.8 bilioni kutokana na mapato ya ndani yatokanayo na
kodi, mapato yasiyo ya kodi na mikopo ya ndani. Kiasi kilichobakia cha
TZS 333.1 bilioni ni kutokana na Washirika wa Maendeleo, ikiwemo kwa
ajili ya Programu na Miradi na Misaada ya Kibajeti. Kwa upande wa
matumizi, jumla ya TZS 307.8 bilioni ziliidhinishwa kwa kazi za kawaida
na TZS 341.1 bilioni kwa ajili ya Programu na Miradi ya Maendeleo.
Mapato ya Ndani
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2012/13 Serikali ilikadiria kukusanya mapato kutokana na vyanzo
vya ndani ya TZS 294.13 bilioni sawa na asilimia 21.3 ya Pato la Taifa.
Kati ya fedha hizo, jumla ya TZS 274.13 bilioni kutokana na vyanzo vya
kodi na TZS 20.00 bilioni ni kutokana na vyanzo visivyokuwa vya kodi.
Kati ya TZS 274.13 bilioni zilizotokana na kodi, Bodi ya Mapato Zanzibar
(ZRB) ilitarajiwa kukusanya kiasi cha TZS 146.00 bilioni. Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ilikadiriwa kukusanya TZS 106.73 bilioni na TZS
21.4 bilioni zilikadiriwa kukusanywa na Idara ya Mhasibu Mkuu wa
Serikali kutokana na Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo
Zanzibar.
20. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
miezi tisa (Julai 2012 hadi Machi mwaka 2013), Serikali ilikadiria
kukusanya mapato ya ndani ya TZS 224.24 bilioni. Makusanyo halisi
yalifikia TZS 201.24 bilioni sawa na asilimia 90 ya makadirio ya kipindi
hicho. Kati ya makusanyo hayo, mapato kutokana na kodi yalifikia TZS
192.41 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 91 ya makadirio wakati mapato
yasiyokuwa ya kodi yalifikia TZS 8.83 bilioni sawa na asilimia 69 ya
makadirio ya kipindi hicho. Yakilinganishwa na makusanyo halisi ya TZS
169.6 bilioni ya kipindi kama hicho mwaka uliopita (2011/12),
kunajitokeza ukuaji wa mapato kwa TZS 31.6 bilioni sawa ongezeko la
asilimia 18.7. Ukusanyaji mapato kitaasisi na kwa kulinganisha na
kipindi kama hicho mwaka uliopita ni kama hivi ifuatavyo:
(i) Mamlaka ya Mapato Tanzania
imekusanya jumla ya TZS 79.51 bilioni sawa na asilimia 99 ya makadirio.
Ukusanyaji huu unamaanisha ukuaji wa mapato wa asilimia 18.5 kutoka TZS
67.1 bilioni;
(ii) Bodi ya Mapato Zanzibar imekusanya
jumla ya TZS 109.48 bilioni sawa na asilimia 85 ya makadirio zikiwemo
TZS 100.65 bilioni za mapato ya kodi sawa na asilimia 87 ya makadirio na
jumla ya TZS 8.8 bilioni zilitokana na mapato ya mawizara. Mapato ya
ZRB yamekuwa kwa asilimia 15.6 kutoka TZS 94.7 bilioni za mwaka jana;
(iii) Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
imekusanya TZS 12.3 bilioni kutokana na Kodi ya Mapato (PAYE) kwa
wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar ambayo ni sawa na asilimia 78 ya
makadirio ya kipindi hicho.
21. Mheshimiwa Spika, matarajio ya sasa
ni kukusanya TZS 269.6 bilioni kutokana na mapato ya ndani hadi kufikia
Juni 2013, sawa asilimia 91 ya makadirio ya mwaka huo. Kati ya mapato
hayo, mapato ya kodi yanatarajiwa kufikia TZS 258.3 bilioni sawa na
asilimia 94 ya makadirio, wakati mapato yasiyokuwa ya kodi yanatarajiwa
kufikia TZS 11.33 bilioni, sawa na asilimia 57 ya makadirio. TRA
inatarajiwa kukusanya jumla ya TZS 105.51 bilioni sawa na asilimia 99 ya
makadirio. Kwa upande wake, ZRB inatarajiwa kukusanya jumla ya TZS
142.68 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 86 ya makadirio na mapato ya
PAYE ni TZS 21.4 bilioni sawa na asilimia 100 ya makadirio.
Mapato ya Nje
22. Mheshimiwa Spika, kati ya TZS 333.2
bilioni zilizotarajiwa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, jumla ya TZS
196.3 bilioni zimepatikana hadi kufikia Machi 2013, zikiwa ni pungufu
ikilinganishwa na TZS 199.05 bilioni zilizopatikana hadi kufikia Machi
2012. Kati ya fedha hizo, TZS 175.8 bilioni ni ruzuku na mikopo kwa
ajili ya Program/Miradi ya Maendeleo ambayo kimsingi haikuongezeka sana
kutoka TZS 174.95 bilioni za mwaka 2011/12. Misaada ya kibajeti imeshuka
hadi kufikia TZS 20.5 bilioni mwaka 2012/13 kutoka TZS 24.1 bilioni
mwaka 2011/12 ambazo ni pungufu kwa asilimia 17.5. Hali hii
imesababishwa na kukwama, kwa sababu za kiutendaji, kwa sehemu ya
Zanzibar ya misaada inayopitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano
DENI LA TAIFA
23. Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa hadi
mwezi wa Machi, 2013 limefikia TZS 252.3 bilioni sawa na asilimia 18.6
ya Pato la Taifa. Deni hili ni sawa na ongezeko la asilimia 20 kutoka
deni la TZS 209.9 bilioni lililoripotiwa katika mwezi wa Machi 2012.
Kati ya deni hilo, deni la ndani ni TZS 48.5 bilioni na lile la nje ni
TZS 203.8 bilioni (USD 128.1 milioni). Kati ya deni la ndani, TZS 3.1
bilioni ni deni la Kiinua Mgongo baada ya kulipa jumla ya TZS 5.8
bilioni kwa wastaafu 617. Matarajio kwa kipindi cha miezi mitatu
iliyobaki ni kuwa deni hili litafikia jumla ya TZS 3.5 bilioni kwa
wafanyakazi watakaostaafu mwezi wa Aprili hadi Juni 2013.
MATUMIZI
24. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza
awali, Serikali ilitarajia kutumia jumla ya TZS 648.3 bilioni kwa mwaka
unaoendelea wa fedha. Kwa miezi tisa, matumizi yote yalitarajiwa kufikia
TZS 434.1 bilioni. Katika kipindi cha tathmini, matumizi halisi
yamefikia jumla ya TZS 428.0 bilioni sawa na asilimia 98.6 ya makadirio
ya miezi tisa au asilimia 66 ya makadirio ya mwaka. Kwa upande wa
matumizi ya fedha za ndani, jumla ya TZS 231.67 bilioni sawa na asilimia
93 ya makadirio ya miezi tisa zimetumika. Kati ya matumizi hayo TZS
205.79 bilioni ni kwa kazi za kawaida sawa na asilimia 97 ya makadirio
ya TZS 212.34 bilioni na TZS 25.88 bilioni ni mchango wa Serikali katika
kazi za maendeleo, sawa na asilimia 71 ya lengo la miezi tisa. Kiasi
kilichobakia cha TZS 196.3 bilioni kimetokana na fedha kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2012/2013
25. Mheshimiwa Spika, Mpango wa
Maendeleo kwa mwaka 2012/13 ulilenga kutekeleza jumla ya programu 38 na
miradi 84 ya maendeleo kupitia klasta tatu zinazounda MKUZA II ambapo
programu sita na miradi 18 ni mipya. Jumla ya TZS 341.1 bilioni
zilitengwa kwa madhumuni hayo. Kati ya fedha hizo TZS 47.9 bilioni sawa
na asilimia 14 ni kutoka Serikalini na TZS 293.2 bilioni sawa na
asilimia 86 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Katika kipindi cha utekelezaji wa Julai -
Machi 2012/13, jumla ya TZS 201.69 bilioni zimetumika kugharamia
utekelezaji wa Programu/Miradi ya Maendeleo ikiwa ni sawa na asilimia 59
ya bajeti yote ya maendeleo. Kati ya fedha hizo TZS 25.88 bilioni ni
mchango wa Serikali sawa na asilimia 54 ya makadirio ya mwaka ya mchango
wa Serikali na TZS 175.81 bilioni ni mchango wa Washirika wa Maendeleo
sawa na asilimia 60 ya makadirio ya fedha kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo.
26. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
utekelezaji ki-Klasta, Klasta ya kwanza ya Ukuzaji Uchumi na Upunguzaji
Umaskini wa Kipato ilitekeleza jumla ya programu 21 na miradi 25 yenye
makisio ya jumla ya TZS 197.9 bilioni sawa na asilimia 58 ya bajeti ya
maendeleo kwa mwaka 2012/13. Fedha zilizotolewa kwa kipindi cha miezi
tisa cha Julai-Machi ni TZS 136.8 bilioni sawa na asilimia 69 ya bajeti
ya Klasta. Kati ya fedha hizo, Serikali imechangia TZS 8.2 bilioni sawa
na asilimia 43.4 ya fedha iliyojipangia na Washirika wa Maendeleo
walichangia TZS 128.6 bilioni sawa na asilimia 71.8 ya fedha
zilizopangwa. Miongoni mwa Miradi mikubwa iliyokamilika chini ya Klasta
hii ni ule wa uwekaji wa njia mpya ya umeme kutoka chini ya Bahari
uliofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Changamoto
za Milenia (MCC). Kwa mara nyengine tena kwa niaba ya Serikali na watu
wa Zanzibar, nawashukuru sana watu wa Marekani na Serikali yao kwa
msaada huu adhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Zanzibar.
27. Mheshimiwa Spika, Klasta ya pili ya
Huduma na Ustawi wa Jamii ilitekeleza jumla ya programu 11na miradi 33
iliyokadiriwa kutumia jumla ya TZS 117.7 bilioni sawa na asilimia 35 ya
bajeti ya maendeleo katika mwaka 2012/13. Fedha zilizotolewa kwa kipindi
cha miezi tisa ni TZS 50.9 bilioni sawa na asilimia 43 ya bajeti ya
Klasta. Kati ya fedha hizo, Serikali imechangia TZS 5.85 bilioni sawa na
asilimia 42.7 ya fedha iliyojipangia na Washirika wa Maendeleo
walichangia TZS 45.07 bilioni sawa na asilimia 43.3 ya fedha
zilizopangwa.
28. Mheshimiwa Spika, Klasta ya tatu ya
Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa ilitekeleza jumla ya programu sita na
miradi 26 yenye jumla ya TZS 25.42 bilioni sawa na asilimia 7.4 ya
bajeti ya maendeleo katika mwaka 2012/13. Fedha zilizotolewa kwa kipindi
cha miezi tisa cha Julai - Machi ni TZS 13.97 bilioni sawa na asilimia
54.9 ya bajeti ya Klasta. Kati ya kiasi hicho, Serikali imechangia TZS
11.82 bilioni sawa na asilimia 77.2 ya fedha iliyojipangia na Washirika
wa Maendeleo walichangia TZS 2.14 bilioni sawa na asilimia 21.2 ya fedha
zilizopangwa.
UTEKELEZAJI MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2012/13
29. Mheshimiwa Spika, Serikali
ilibainisha maeneo mbalimbali ya kipaumbele katika katika Bajeti yake ya
mwaka 2012/13. Maeneo hayo ni pamoja na Kuimarisha huduma za afya;
Kuimarisha ajira kwa vijana; Kuimarisha ustawi wa wazee; Kuimarisha
elimu ya lazima; Kuimarisha uchumi; na Kuimarisha mashirikiano ya Sekta
Binafsi na Umma. Tumeendelea kupiga hatua katika kuyafikia malengo yetu.
Hata hivyo, utekelezaji umefikia viwango tofauti baina ya Sekta.
Maelezo kamili ya hatua iliyofikiwa kwa kila eneo yatatolewa na
Waheshimiwa Mawaziri husika katika Hotuba zao za Bajeti.
SENSA YA WATU NA MAKAAZI
30. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa
nchi yetu ilifanya Sensa ya Watu na Makaazi katika mwezi wa Agosti mwaka
2012. Serikali ilifanya jitihada maalum kuwaelimisha wananchi juu ya
umuhimu wa Sensa. Matokeo ya Sensa hii yalitangazwa rasmi na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 31/12/2012. Matokeo hayo
yameonesha kuwa nchi yetu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa ina
jumla ya wakaazi 44,928,923. Sensa pia imebainisha kuwa idadi yetu
katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba imefikia watu 1,303,569 ambapo
watu 896,721, sawa na asilimia 69, wanaishi Unguja na watu 406,868, sawa
na asilimia 31 ya watu wote wa Zanzibar, wanaishi katika kisiwa cha
Pemba.
31. Mheshimiwa Spika, Matokeo haya ya
Sensa pia yanaashiria kuwa idadi ya watu Zanzibar imekuwa ikiongezeka
kwa wastani wa asilimia 2.8 kwa mwaka tokea Sensa ya mwaka 2002. Pamoja
na kupungua kwa kasi yetu ya ukuaji wa idadi ya watu kutoka asilimia 3.1
kwa mwaka baina ya Sensa zilizopita, bado kiwango hiki cha asilimia 2.8
ni kikubwa na jitihada zaidi zinahitajika ili kukidhibiti. Kwa upande
mwengine, Sensa pia imebainisha changamoto nyengine muhimu ambayo ni
mkusanyiko mkubwa wa watu katika miji yetu. Kwa mujibu wa takwimu za
Sensa, karibu nusu ya Wazanzibari wote, yaani asilimia 46, sawa na watu
593,678, wanaishi katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Kwa kuzingatia ukubwa
wa Mkoa wenyewe, idadi hiyo ya wakaazi inafanya wakaazi wa kila kilomita
moja ya mraba kwa mkoa huu kuwa ni watu 2,581 ambayo ni ya pili kwa
ukubwa kwa Tanzania ikitanguliwa na Dar Es Salaam yenye wastani wa
wakaazi 3,133 kwa Kilomita ya Mraba. Uchambuzi muhimu wa takwimu za
Sensa unaendelea na matokeo yake yataendelea kutolewa kwa awamu.
MAANDALIZI YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO
32. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba
yangu ya mwaka jana nilizungumzia pia mchakato wa uandaaji wa Katiba
mpya ya Jamhuri yetu ya Muungano na kuwanasihi wananchi WOTE kujiepusha
na vitendo vya uvunjifu wa amani. Niliwaomba kustahamiliana pale
tunapokuwa na mitazamo inayotofautiana. Nawashukuru wananchi walio wengi
kwa kuisikiliza Serikali na kuwa watulivu. Hata hivyo, sio wote
walikuwa na busara na hekima ya ustahamilivu. Wakati kwa ujumla mchakato
wa ukusanyaji wa maoni juu ya Katiba hiyo umekwenda vizuri,
kulijitokeza matukio yasiyopendeza na ya kuhatarisha amani. Tunashukuru
hali imetulia kwa sasa lakini lazima tutumie uzoefu wa mchakato huo
kujifunza. Tunahitaji kukuza demokrasia yetu kwa ustaarabu wa kuruhusu
misimamo na mitazamo tofauti miongoni mwetu. Mchakato wenyewe wa kuipata
hiyo Katiba mpya unaendelea. Mafunzo tuliyoyapata katika hatua ya
ukusanyaji wa maoni yatuongoze vyema katika hatua zitakazofuata hadi
kukamilika kwake.
33. Mheshimiwa Spika, tayari Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imeshatoa Rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Kuna hatua nyengine kadhaa hadi kupatikana kwa
Katiba mpya kama zilivyooneshwa katika Sheria ya Tume hiyo. Ni wajibu wa
kila mmoja wetu na sote kwa pamoja kuhakikisha kwamba mageuzi haya
muhimu katika nchi yetu hayatufarakanishi, sio wenyewe kwa wenyewe
miongoni mwetu Wazanzibari wala baina yetu na ndugu zetu wa Tanzania
Bara. Kwa vyovyote vile, kwa kuzingatia historia, muingiliano na ukaribu
wa nchi zetu bado tunahitajiana baina yetu na Tanzania Bara. Bado
tunahitaji ujirani ulio mwema na wa mashirikiano hata kama tungekuwa
nchi tofauti, seuze leo tumo katika Jamhuri moja ya Muungano.
Tukamilishe basi mchakato wa kupatikana Katiba mpya tukiendelea kuwa
wamoja na ndugu.
34. Mheshimiwa Spika, baada ya mapitio
hayo ya utendaji wetu wa miezi tisa ya mwanzo ya mwaka 2012/13, naomba
sasa nieleze kwa mukhtasari mwelekeo wa Hali ya Uchumi kwa mwaka 2013 na
Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14.
MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI
35. Mheshimiwa Spika, kuwepo kwetu hapa
leo na demokrasia tunayojinasibisha nayo ni matokeo ya kazi kubwa na ya
kishujaa iliyofanywa na wazee wa Taifa letu ambao walijumuika na
kujitolea muhanga ili kizazi chetu kiwe huru na kuweza kujiamulia
wenyewe mambo yake na kujiletea maendeleo. Matokeo ya kujitolea kwao
muhanga ni Mapinduzi matukufu ya tarehe 12 Januari 1964. Tukijaaliwa,
tarehe kama hiyo mwakani tutaadhimisha kutimia kwa mwaka wa 50 tokea
kugombolewa kwa Zanzibar yetu. Hii ni siku adhimu na itahitaji
maadhimisho yanayofanana nayo. Serikali imejipanga na kujiandaa vyema na
maadhimisho hayo.
MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI 2013
Uchumi wa Dunia na wa Kanda
36. Mheshimiwa Spika, uchumi wa dunia
unatarajiwa kukua kufikia asilimia 3.3 mwaka 2013 ikilinganishwa na
ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka 2012. Hali hii ya ukuaji mzuri
inatarajiwa pia katika kila Kanda kama ifuatavyo :
(i) Kwa nchi zilizoendelea ukuaji unatarajiwa kufikia asilimia 1.2 mwaka 2013 kama ilivyokuwa mwaka 2012.
(ii) Kwa nchi zinazoendelea na
zinazoibuka kiuchumi uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.3 kwa mwaka
2013 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2012;
(iii) Uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara unatarajiwa kuimarika zaidi kwa kukua kwa asilimia 5.6
mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2012.
MFUMKO WA BEI WA DUNIA
37. Mheshimiwa Spika, kasi ya mfumko wa
bei duniani unatarajiwa kushuka kufikia asilimia 3.1 kwa mwaka 2013
ukilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2012. Nchi zilizoendelea, kasi ya
mfumko wa bei inatarajiwa kupanda kufikia asilimia 1.4 kwa mwaka 2013
ikilinganishwa na asilimia 1.3 mwaka 2012. Aidha, mfumko wa bei kwa nchi
zinazoendelea na zinazoibuka kiuchumi hautakuwa na mabadiliko
unatarajiwa kuwa asilimia 5.9 kwa mwaka 2013 kama ilivyokuwa mwaka 2012.
Hata hivyo, mfumko wa bei kwa nchi za Kusini ya Jangwa la Sahara
unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 7.2 mwaka 2013 ukilinganishwa
na asilimia 9.1 mwaka 2012.
HALI YA UCHUMI WA ZANZIBAR
38. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013
uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kuendelea kuimarika na kukua kwa asilimia
7.5 kutoka ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2012.
Matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2013 yanatokana na mambo yafuatayo:
(i) Kukamilika kwa uwekaji wa waya wa umeme wa chini ya bahari kutoka Rasi Kiromoni Tanzania Bara hadi Rasi Fumba.
(ii) Kuimarika kwa sekta ya utalii
kutokana na kupanuka kwa wigo wa bidhaa na huduma za utalii zinazofanywa
na wajasiri amali, vile vile kukuza na kutangaza utalii katika soko la
ndani na nje ya nchi kwa dhana ya utalii kwa wote.
(iii) Kuendelea kuimarika kwa vyanzo vya mapato.
(iv) Utekelezaji wa program ya mapinduzi ya kilimo Zanzibar.
(v) Kuendelea kuimarika kwa mashirikiano baina ya sekta za Umma na Binafsi.
(vi) Kupatikana kwa mkongo (fiber optic) ambao utarahisisha shughuli za huduma ya mawasiliano.
(vii) Kuvutia wawekezaji katika kuimarisha maendeleo ya viwanda vidogo vidogo nchini.
(viii) Kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na ufugaji wa mazao ya baharini.
(ix) Kuendelea kwa uwekezaji katika kuimarisha miundombinu hasa ya barabara na viwanja vya ndege.
(x) Kuendelea na jitihada za usambazaji wa umeme vijijini na visiwa vidogo vidogo.
(xi) Kuendelea kuimarika kwa amani na utulivu wa kisiasa.
Mfumko wa Bei
39. Mheshimiwa Spika, mfumko wa bei
unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 7.9 mwaka 2013 ukilinganishwa
na asilimia 9.4 mwaka 2012. Matarajio hayo ya kushuka kwa kasi ya mfumko
wa bei yanatokana na:
(i) Kushuka kwa mfumko wa bei duniani;
(ii) Kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa mazao ya chakula na biashara;
(iii) Kuimarika kwa Sekta ya Uvuvi; na
(iv) Kuendelea na utulivu wa sarafu ya Tanzania.
MWELEKEO WA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2013/14
40. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/14
Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo utazingatia zaidi utekelezaji wa Dira ya
Maendeleo 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA
II), Utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa MKUZA II, Malengo ya
Maendeleo ya Milenia ya mwaka 2015 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010.
MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2013/14
41. Mheshimiwa Spika, haitarajiwi kwamba
vipaumbele vya Serikali viwe vinabadilika sana mwaka hadi mwaka. Mengi
ya maeneo ya kipaumbele yanahitaji uwekezaji wa muda mrefu ili kufikia
malengo ya maendeleo ya nchi. Tunahitaji kujenga Taifa lenye maendeleo
makubwa ya kiuchumi; lenye watu walioelimika, wataalamu wenye hadhi ya
kimataifa na wenye siha na wasiosumbuliwa na maradhi yanayoepukika. Kwa
kuzingatia ukweli huu, bado kipaumbele cha Serikali kitaendelea kuwa
katika kukuza kwa kasi zaidi uchumi wetu na kuongeza ajira, hususan kwa
vijana, kuimarisha ubora wa elimu, kuimarisha huduma za afya hususan
katika upatikanaji wa dawa za lazima na katika upatikanaji wa maji safi
na salama. Maeneo haya yote yataendelea kujitokeza kama kipaumbele kwa
miaka ijayo ya fedha.
42. Mheshimiwa Spika, ajira itaendelea
kuimarishwa kupitia Program mbalimbali za uwekezaji kama vile katika
Kilimo, Viwanda na Utalii. Jambo la msingi ni kuhakikisha uendelevu wa
ukuaji wa uchumi, kwa kasi kubwa zaidi na kwamba ukuaji huo lazima
utafsirike katika kuleta ajira bora. Kuhusu elimu, Sekta hii inapaswa
kuwa kipaumbele cha Taifa kwa muda wote. Mafanikio makubwa tayari
yamefikiwa katika usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu hadi
ngazi ya sekondari. Kipaumbele cha serikali katika sekta hii muhimu
kitaendelea kuwa katika kuimarisha ubora wake. Kwa upande wa afya, bado
upatikanaji wa dawa na visaidizi (sundries) utaendelea kupata umuhimu
maalum. Kwa upande mwengine, Serikali inatambua shida wanayoipata
wananchi katika maeneo mbalimbali kuhusiana na upatikanaji wa maji safi
na salama. Mkazo utaendelea kuwekwa katika kuhakikisha kuwa huduma hii
ya lazima kwa uhai inapatikana kwa wananchi walio wengi.
43. Mheshimiwa Spika, mambo yote haya
yatafanyika bila ya kupuuza umuhimu wa miundombinu ya msingi kama vile
barabara, bandari, viwanja vya ndege, umeme ikiwemo kutafuta chanzo
mbadala cha nishati hiyo, kwa maendeleo ya nchi yetu. Katika Mpango wa
Maendeleo wa mwaka ujao wa Fedha, Miundombinu ya Barabara, Viwanja vya
ndege na Bandari imepangiwa jumla ya TZS 62.7 bilioni, ile ya Kilimo na
Ufugaji jumla ya TZS 15.0 bilioni na ya Nishati jumla ya TZS 9.6
bilioni.
44. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba
wakati tukiendelea na bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13, nilitoa
kauli ya Serikali juu ya ahadi yake ya ununuzi wa meli mpya ya abiria na
mizigo. Sote kwa pamoja tulikubaliana na haja ya kujibana katika
matumizi, kwa kukata bajeti ya Wizara zote, ili kupatikana fedha kwa
madhumuni hayo. Kwa bahati mbaya, mchakato wa kupata mjenzi wa meli hiyo
umehitaji muda mrefu kukamilika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
Serikali imeamua kujenga meli hiyo badala ya kununua meli iliyotumika.
Aidha, kwa maumbile yake, suala hili limehitaji majadiliano ya kina ya
kiufundi, kifedha na kisheria. Hata hivyo, nina furaha kulijulisha
Baraza lako Tukufu kuwa hatimae mchakato huu umepiga maendeleo mazuri na
tayari mkataba wa ujenzi umeshatayarishwa na unatarajiwa kutiwa saini
mwezi huu baina ya SMZ na Kampuni ya Daewoo International ya Korea ya
Kusini. Meli hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za
mizigo itagharimu Dola za Kimarekani 30.4 milioni sawa na TZS 48.6
bilioni na inatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miaka miwili na kuwasili
nchini mwezi Juni 2015.
45. Mheshimiwa Spika, naomba nitaje kwa
ufupi jinsi maeneo ya kipaumbele yalivyozingatiwa katika Bajeti ya
Maendeleo kama ifuatavyo:
(i) Jumla ya TZS 55.4 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Miradi ya Maji safi na salama;
(ii) Sekta ya Elimu imetengewa TZS 32.8 bilioni;
(iii) Sekta ya Afya imetengewa jumla ya TZS 23.9 bilioni; na
(iv) Programu ya Ajira kwa Vijana
imetengewa TZS 1.1 bilioni kwa ajili ya ajira ya moja kwa moja, zaidi ya
ile inayotokana na utekelezaji wa Programu na Miradi mbalimbali kama
nilivyoeleza awali.
Kwa ujumla, katika Bajeti ya mwaka ujao
wa fedha, maeneo haya manne tu ya kipaumbele yametengewa jumla ya TZS
113.2 bilioni kati ya TZS 305.4 bilioni. Kiasi hiki ni zaidi ya theluthi
moja ya Bajeti yote ya Mpango wa Maendeleo, sawa na asilimia 37 ya
Bajeti hiyo. Kwa kuzingatia kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji
kinachotengwa kwa ajili ya huduma hizo, bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni
Bajeti ya Huduma za Jamii kwa wananchi wa Zanzibar.
46. Mheshimiwa Spika, sambamba na
vipaumbele hivyo, maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa Dira ya 2020 na
MKUZA II yamewekwa katika Programu tano kubwa kama ifuatavyo:
A. Programu ya Mageuzi ya Kiuchumi
Programu hii inakusudia kuziimarisha sekta ya utalii, biashara, viwanda na kilimo.
B. Programu ya Mageuzi ya Serikali
Programu hii ina lengo la kuimarisha
Utawala Bora, Uwajibikaji na utoaji huduma kwa matokeo kwa utendaji, na
utoaji huduma wa Serikali kwa kupima viashiria vya msingi vya utendaji
(KPIs); kupambana na rushwa na kujenga uwezo.
C. Programu ya Kujenga Uwezo wa Rasilimali Watu
Kwa upande wa Kujenga Uwezo wa Rasilimali watu maeneo yatakayozingatiwa ni kuimarisha huduma za afya na ubora wa elimu.
D. Masuala Mtambuka
Kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, maafa na uhifadhi wa mazingira, jinsia na watu wenye mahitaji maalum.
E. Visaidizi (enablers)
Kwa utekelezaji wa mageuzi
yaliyotangulia Serikali itahitaji viwezeshaji muhimu vitakavyojumuisha
uimarishaji wa miundombinu, kukuza ujuzi wa kazi na ujasiriamali, ubora
na viwango na mkakati wa kuendeleza sekta binafsi.
RASILIMALI KWA AJILI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2013/14
47. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2013/14 Serikali inatarajia kutekeleza jumla ya Programu 35, moja ikiwa
ni mpya, na Miradi 75 ya maendeleo ambapo tisa ni mipya. Jumla ya TZS
305.4 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa kutekeleza Programu na Miradi
hiyo. Kati ya fedha hizi, Serikali itatoa TZS 70.0 bilioni na Washirika
wa Maendeleo watachangia TZS 235.4 bilioni ikiwemo ruzuku ya TZS 86.8
bilioni na mikopo TZS 148.6 bilioni.
MAANDALIZI YA BAJETI INAYOZINGATIA PROGRAMU
48. Mheshimiwa Spika, kwa miaka miwili
sasa Serikali imeendelea na matayarisho ya maandalizi ya mageuzi ya
mfumo wa bajeti yenye lengo la kuimarisha uandaaji, utekelezaji na
usimamizi wa bajeti na unaosisitiza matokeo kutokana na matumizi ili
kuleta ufanisi katika utekelezaji wa bajeti. Mfumo huu umeanza
kutekelezwa kwa majaribio mwaka huu 2012/13 na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo na Maliasili, Wizara
ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano
na Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Majaribio hayo
yamehusu kutayarisha Muundo na Maelezo ya Programu yenye kuhusisha
malengo, matokeo, viashiria, shabaha na gharama za Programu. Maelezo
hayo yaliwasilishwa sambamba na mfumo wa sasa wa bajeti. Kwa Bajeti za
mwaka ujao wa fedha wa 2013/14, wizara zote zilizobakia nazo zimeingia
katika maandalizi hayo ya mfumo mpya wa Bajeti kwa kuhusisha maeneo
yaliyotajwa. Matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2014/15 Bajeti ya
Serikali iwe inaandaliwa na kutekelezwa kwa kuzingatia mfumo huo wa
Programu.
MWELEKEO WA BAJETI 2013/14
SURA YA BAJETI
Mapato
49. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatarajia kutumia jumla ya TZS 658.5 bilioni katika mwaka wa fedha
2013/14 ikimaanisha ongezeko dogo la asilimia 1.5 kutoka Bajeti ya TZS
648.9 bilioni mwaka 2012/13. Kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa mapato
kutokana na vyanzo vya ndani, inatarajiwa kuwa mapato ya ndani yatafikia
jumla ya TZS 333.7 bilioni na hivyo kufanya jumla ya mapato hayo
kufikia TZS 338.7 bilioni ikichanganywa na TZS 5.0 bilioni
zinazotarajiwa kusalia mwisho wa mwaka. Mapato ya ndani yanahusisha
mapato ya Kodi na yasiyo ya kodi, ikiwemo gawio kutoka Benki Kuu na
Mashirika ya Serikali. Ikilinganishwa na matumizi yanayotarajiwa kama
nilivyoyataja, kiasi hicho cha mapato cha TZS 338.7 bilioni kitaacha
nakisi ya TZS 310.5 bilioni.
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka huo
wa 2013/14, Serikali inatarajia kupokea jumla ya TZS 277.9 bilioni
kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Fedha hizi zinajumuisha TZS 235.4
bilioni za Mikopo na Ruzuku kwa Programu na Miradi ya Maendeleo, TZS
40.0 bilioni za Msaada wa Kibajeti na TZS 2.5 bilioni kutokana na
msamaha wa madeni (MDRI). Yakichanganywa na mapato ya ndani, jumla ya
mapato yote ya Serikali inafikia TZS 616.6 bilioni. Kwa kuzingatia
matumizi yote ya Serikali ya TZS 658.5 bilioni mapato haya yanaacha
nakisi ya TZS 41.9 bilioni.
51. Mheshimiwa Spika, ili kuziba pengo
hilo la Bajeti, Serikali inakusudia kuchukua hatua mbalimbali za
kuimarisha mapato ya ndani kwa kurekebisha viwango vya kodi na ada za
huduma mbalimbali. Kwa ujumla, hatua hizo zinatarajiwa kuingiza TZS 16.9
bilioni, na hivyo kuzidi kupunguza pengo la bajeti na kufikia TZS 25.0
bilioni. Serikali inakusudia kukopa ndani kwa kiwango hicho cha TZS 25
bilioni na hivyo kuleta uwiano wa mapato na matumizi katika Bajeti.
Matumizi
52. Mheshimiwa Spika, kati ya matumizi
ya TZS 658.5 bilioni yanayotarajiwa kwa mwaka 2013/14, TZS 353.1 bilioni
sawa na asilimia 53.6 ni kwa ajili ya kazi za kawaida na TZS 305.4
bilioni sawa na asilimia 46.4 ni kwa kazi za maendeleo. Itakumbukwa pia
kuwa Serikali, kupitia kwa Mheshimiwa Rais, iliahidi kuimarisha kipato
cha Mfanyakazi kila hali ya uchumi na uwezo wa serikali inaporuhusu.
Katika kutekeleza ahadi hiyo, marekebisho makubwa ya maslahi ya
wafanyakazi yalifanyika kuanzia mwezi Oktoba 2011. Ahadi ya Mheshimiwa
Rais bado ipo na itaendelea kutekelezwa kama alivyoahidi. Kwa azma hiyo,
katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inakusudia kuimarisha tena maslahi
ya wafanyakazi. Jumla ya TZS 17.5 bilioni zimetengwa kwa madhumuni hayo
na kuhudumia na ajira mpya na marekebisho mengine muhimu. Kwa kutambua
mchango mkubwa wa Baraza lako, marekebisho pia yamefanywa kwa maslahi ya
Wajumbe wako ambao nao wana majukumu mengi.
53. Mheshimiwa Spika, matumizi
yaliyotajwa hapo juu ya TZS 658.5 bilioni ni jumla tu ya mtumizi yote.
Matumizi haya yanahusisha pia yale ya lazima, kwa mujibu wa Sheria, na
mengine ambayo tayari Serikali yetu ilikwishajifunga na hivyo ni lazima
yafanyike. Miongoni mwa matumizi ya lazima (Mandatory Expenditure) ni
haya yafuatayo:
(i) Mishahara (pamoja na ruzuku) TZS 176.3 bilioni.
(ii) Malipo ya Kiinua Mgongo na Pencheni – TZS 20.6 bilioni.
(iii) Malipo ya Dhamana za Hazina na Hati Fungani – TZS 14.5 bilioni
(iv) Huduma za Viongozi wakuu, Hospitali na chakula cha vikosi– TZS 11.5 bilioni.
(v) Mchango wa Washirika wa Maendeleo kwa Programu na Miradi ya Maendeleo – TZS 235.4 bilioni.
(vi) Mchango wa SMZ kwa Programu na Miradi ya Maendeleo inayoendelea na ambayo ina mikataba yenye thamani TZS 56.0 bilioni.
(vii) Mahitaji ya dawa, vifaa vidogo vidogo (sundries) pamoja na dawa za maabara zenye thamani ya TZS 2.1 bilioni.
54. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, kiasi
cha TZS 516.4 bilioni tayari zina matumizi maalum na haziwezi
kugawanywa. Hali hii inabakisha TZS 142.1 bilioni ambazo ndio
zimegawanywa kwa ajili ya kazi za kawaida kwa Serikali na taasisi zake
zinazopokea ruzuku, matumizi ya Mfuko Mkuu wa Serikali na mchango wa
Serikali kwa miradi mingine ya maendeleo.
55. Mheshimiwa Spika, pamoja na
kuendelea kusisitiza kuchukua hatua za kuimarisha mapato, Serikali pia
inaendelea na hatua maalum zinazolenga kuangalia uwezekano wa kubana
matumizi kwa kazi za kawaida bila ya kuathiri utendaji. Lengo ni kuwa
kama kuna fedha zitakazookolewa, fedha hizo zitumike kwa kazi za
maendeleo. Kwa sasa, zoezi la kufanya mapitio ya majukumu ya kila
Wizara/Taasisi linaendelea. Kukamilika kwake kunatarajiwa kusaidia
kuongeza ufanisi kupitia marekebisho ya kitaasisi na kuepusha mgongano
wa kimajukumu.
MAPENDEKEZO YA HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO
56. Mheshimiwa Spika, moja ya lengo la
Serikali ni kuhakikisha utulivu wa mfumo wa kodi ili uwe wenye
kutabirika na hivyo kuvutia uwekezaji. Hatua za kuongeza kodi
huchukuliwa pale tu inapokuwa ni lazima. Kwa upande mwengine, sasa hivi,
kuliko ilivyokuwa kwa wakati mwengine wowote ule, haja ya kupunguza
utegemezi wa wafadhili inajitokeza. Changamoto zinazojitokeza kutokana
na athari ya msukosuko wa kiuchumi na fedha katika eneo la Ulaya na
kukua kwa mahitaji ya huduma kwa wananchi na dhamira ya Serikali ya
kuimarisha ubora wa huduma hizo kunapelekea haja ya kuimarisha zaidi
mapato yetu ya ndani. Kwa kuzingatia mambo yote haya muhimu, na ili
kuziba nakisi ya bajeti katika mwaka ujao wa fedha 2013/14 kama
nilivyoeleza awali, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya sheria
na viwango vya kodi na ada mbalimbali kwa kurekebisha Sheria zifuatazo:
(i) Sheria ya VAT, namba 4 ya mwaka 1998.
(ii) Sheria ya Kodi za Hoteli namba 1 ya mwaka 1995.
(iii) Sheria ya Ada za Bandari namba 2 ya mwaka 1999.
(iv) Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 6 ya mwaka 1996.
(v) Sheria ya Kodi za Mafuta namba 7 ya mwaka 2001.
(vi) Sheria ya Usafiri wa Barabara namba 7 ya mwaka 2003 na Kanuni zake.
(vii) Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 (Presumptive Tax Scheme).
(viii) Sheria ya Ardhi namba 12 ya mwaka 1992.
(ix) Sheria ya Kuvutia na Kulinda Vitega Uchumi namba 11 ya mwaka 2004.
(x) Sheria ya Usimamizi wa Kodi namba 7 ya mwaka 2009.
(xi) Sheria ya Rufaa ya Kodi namba 1 ya mwaka 2006.
A. Marekebisho ya Sheria ya VAT
57. Mheshimiwa Spika, pamoja na
mafanikio ya uwekezaji katika sekta ya utalii na mchango wake mkubwa
katika uchumi wa nchi yetu, bado kumekuwa na udanganyifu katika ulipaji
wa kodi zinazotokana na sekta hii. Baadhi ya Wawekezaji wameendelea
kudanganya kuhusu kiasi wanachopaswa kulipa kwa kutaja kiwango kidogo
cha kutozea kodi kwa mahoteli. Pamoja na hatua mbalimbali za kisheria na
kiutawala zilizochukuliwa na Serikali ili kurekebisha hali hii, bado
kuna fursa ya kuimarisha zaidi mapato hayo ikiwemo kwa kudhibiti zaidi
msingi wa kutozea kodi. Kwa mnasaba huo, inapendekezwa kurekebisha
kiwango cha usajili wa mahoteli katika kodi ya VAT kwa kuzisajili tu
hoteli zinazofikia kiwango cha chini cha usajili wa VAT na zenye kutoza
ada ya huduma kuanzia USD 100 kwa mtu kwa siku (au sawa na thamani hiyo
kwa Shilingi za Kitanzania). Hoteli nyengine zote zisizofikia kiwango
hicho zitalipa Kodi ya Hoteli (Hotel Levy).
58. Mheshimiwa Spika, nchi nyingi
zinapata tabu juu ya udhibiti wa udanganyifu katika misamaha ya kodi.
Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada za kudhibiti misamaha ya kodi
lakini bado kuna fursa ya kudhibiti zaidi. Chini ya utaratibu wa sasa wa
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Serikali hutoa unafuu kwa Taasisi
mbalimbali chini ya Jadweli la Tatu la Sheria ya VAT. Ili kukabiliana na
udanganyifu na kuimarisha zaidi udhibiti wa misamaha, inapendekezwa
kupunguza unafuu unaotolewa kwa baadhi ya Taasisi. Unafuu wa asilimia
100 ubakie tu kwa ofisi za Kibalozi na Miradi yenye ufadhili wa
Washirika wa Maendeleo, vifaa na huduma zinazostahili. Kwa Taasisi
nyengine zote zinazostahiki msamaha huo chini ya Jadueli hilo unafuu
utolewe kwa asilimia 80 tu ili kiasi kilichobakia cha asilimia 20
kilipiwe kodi.
Kwa kuzingatia na hatua nyengine za
kiutawala zitazochukuliwa katika VAT, hatua hiyo inatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa TZS 4.56 bilioni.
B. Marekebisho ya Sheria ya Kodi za Hoteli
59. Mheshimiwa Spika, sambamba na
marekebisho ya Sheria ya VAT, inapendekezwa pia kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi za Hoteli kwa kutoza kodi kwa kuzingatia hadhi ya
hoteli. Inapendekezwa kuwa hoteli zote zinazotoa huduma kwa kiwango
kisichozidi Dola za Kimarekani (USD) 45 kwa mgeni kwa siku ziendelee
kulipa VAT kwa kiwango maalum (specific). Hata hivyo, inapendekezwa
kupandisha kiwango hicho kutoka USD 5 kwa mtu kwa siku ya sasa hadi USD
8. Hoteli zilizobakia zinazotoza zaidi ya USD 45 lakini hazitimizi sifa
ya kusajiliwa chini ya VAT zitaendelea kutozwa Kodi ya Hoteli kwa
kiwango cha asilimia 18 kama ilivyo sasa. Marekebisho haya yanatarajiwa
kuiingizia Serikali jumla ya TZS 2.86 bilioni.
C. Kurekebisha Sheria ya Ada ya Viwanja vya Ndege
60. Mheshimiwa Spika, marekebisho
yanayopendekzwa kufanywa katika Sheria hii yanalenga kuleta uwiano baina
ya kiwango kinachotozwa Zanzibar cha ada ya uwanja wa ndege na viwango
vinavyotozwa katika nchi nyengine za Afrika ya Mashariki. Inapendekezwa
kupandisha ada hiyo kutoka USD 35 kwa mtu iliyopo sasa hadi USD 40 kwa
mtu kama ilivyo kwa nchi jirani za Afrika ya Mashariki. Marekebisho haya
yatagusa tu wasafiri waendao nje ya nchi. Kwa wasafiri wa ndani ya
nchi, kiwango cha sasa kitaendelea kutumika kama kilivyo. Matarajio ni
kwamba hatua hiyo itaongeza mapato kwa TZS 1.2 bilioni.
D. Marekebisho ya Ushuru wa Stempu
61. Mheshimiwa Spika, Sheria hii
ilifanyiwa marekebisho ya viwango mwaka jana. Hata hivyo, wakati wa
utekelezaji, imebainika haja ya Serikali kuangalia tena unafuu wa kodi
unaotolewa kwa bidhaa za vyakula muhimu. Kwa upande mwengine,
kumejitokeza pia ugumu wa utekelezaji katika maeneo ya baadhi ya hati
zinazopaswa kulipiwa Ushuru wa Stempu. Ili kuondoa kasoro
zilizojitokeza, marekebisho yafuatayo yanapendekezwa:
(i) Kushusha rasmi kiwango cha Ushuru wa
Stempu kwa bidhaa za mchele na unga wa ngano kutoka asilimia 3 cha sasa
hadi asilimia 2;
(ii) Aidha, inapendekezwa kupanua ukomo
wa kiwango cha malipo ya ushuru huu uliotolewa mwaka jana kwa mikopo ili
utumike kwa hati nyengine zenye hadhi ya mikopo kama vile “Debentures”.
Kwa utaratibu huu, marekebisho yataweka kiwango cha juu cha Ushuru huu
cha TZS 100,000.
(iii) kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Stempu kulingana na utaratibu wa “Presumptive Tax” kama unavyopendekezwa hapa chini.
62. Mheshimiwa Spika, sambamba na
marekebisho hayo ya sheria, Serikali kupitia ZRB inakusudia kuchukua
hatua kadhaa za kiutawala zikiwemo za kuanzisha ofisi za ZRB katika
Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja ili kuweza kuhudumia kwa karibu
zaidi walipakodi waliopo katika maeneo hayo na kutoa uwakala wa zuio la
Ushuru wa Stempu (withholding Tax) kwa hoteli mbalimbali. Tayari ZRB
inazo ofisi katika miji ya Chakechake, Wete na Mkoani kwa Pemba. Kwa
pamoja hatua hizi zinategemewa kuingiza jumla ya TZS 600.0 milioni.
E. Kuimarisha utaratibu wa utozaji kodi ya mafuta
63. Mheshimiwa Spika, kumeendelea kuwepo
upotevu wa mapato ya Serikali kupitia magendo katika biashara ya
mafuta. Hali hii haiwezi kuachwa iendelee. Serikali kupitia TRA, ZRB na
vikosi vya ulinzi itafanya operesheni maalum na ya kudumu ya kudhibiti
magendo na vituo visivyo rasmi ya kuuzia mafuta. Aidha, ili kudhibiti
uingiaji wa mafuta ya magendo, makubaliano ya msingi yamefikiwa baina ya
TRA/ZRB na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) ya kuanzisha utaratibu
rasmi wa kubadilishana taarifa za uingizaji wa mafuta. Lengo ni kuzuia
udanganyifu unaofanywa na waingizaji wasio waaminifu na hivyo kuchangia
katika kuwepo kwa magendo. Matarajio ni kwamba hatua hizi zitaongeza
mapato ya TZS 5.0 bilioni. Sambamba na hatua hizo, ili kuzuia uwezekano
wa udanganyifu na kuhakikisha kuwepo kwa bidhaa hiyo muhimu kwa muda
wote, Serikali itafanya upembuzi yakinifu juu ya uwezekano na utaratibu
bora wa kuwa na muingizaji mmoja tu wa mafuta (single importer), kama
ilivyokuwa kabla.
F. Marekebisho ya utaratibu wa malipo ya leseni ya njia
64. Mheshimiwa Spika, moja ya msingi
muhimu wa kutoza kodi ni kuwa kodi ilipwe kwa kuzingatia matumizi na
faida inayopatikana kutokana na matumizi ya huduma husika (benefit
principle). Utaratibu wa sasa wa malipo ya matumizi ya barabara
hauzingatii msingi huu muhimu na unawezesha kuwepo kwa leseni bandia za
njia na hivyo kuikosesha mapato serikali. Ili kukabiliana na kasoro
hizo, inapendekezwa kubadilisha utaratibu wa ukusanyaji wa ada hiyo kwa
kuiingiza katika mafuta. Kwa kuzingatia wastani wa matumizi ya kawaida
na bila ya kumuongezea mzigo mtumiaji wa kawaida wa barabara,
inapendekezwa kutozwa TZS 35 kwa lita ya dizeli au petrol itakayouzwa
nchini kama leseni ya njia. Kwa kuwa kiwango hicho hakitaongeza mapato
(revenue neutral), hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato kwa TZS 124
milioni tu kutokana na udhibiti wa leseni bandia na ucheleweshaji wa
sasa wa malipo.
G. Marekebisho ya viwango vya malipo ya leseni za udereva
65. Mheshimiwa Spika, kwa muda sasa
Zanzibar imekuwa ikitumia leseni za kisasa za udereva ambazo gharama za
utengenezaji wake zimeendelea kupanda. Ili kufidia gharama zinazotumika
kutayarisha nyaraka za leseni za udereva na leseni hizo za kisasa kuwa
endelevu, inapendekezwa kurekebisha kiwango cha leseni za udereva kutoka
TZS 15,000 hadi TZS 20,000 kwa leseni ya mwaka mmoja, TZS 25,000 hadi
TZS 30,000 kwa leseni ya miaka miwili na TZS 35,000 hadi TZS 40,000 kwa
leseni ya miaka mitatu. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa TZS 120 milioni.
H. Kuweka utaratibu wa kusajili magari mara tu yanakapoingia nchini
66. Mheshimiwa Spika, kutokana na
kuimarika kipato cha wananchi na biashara, kumejitokeza kushamiri kwa
biashara ya magari hapa nchini katika sehemu mbalimbali. Kwa bahati
mbaya, kumejitokeza mtindo wa baadhi ya watu kutembelea magari hayo bila
ya kutiwa nambari za usajili. Tabia hii ikiachiliwa inaweza kuathiri
usalama wa watumiaji wa barabara (safety) na pia kuongeza vitendo vya
uhalifu. Ili kukabiliana na hali hiyo, kuanzia mwaka ujao wa fedha,
vyombo vya moto vitasajiliwa mara tu vinapokamilisha taratibu za Forodha
na kabla ya kutoka bandarini. Sambamba na hatua hiyo, mambo yafuatayo
yanapendekezwa:
(a) Kuongeza kiwango cha usajili
(registration) wa vyombo vya moto kutoka TZS 50,000 hadi TZS 70,000, na
hivyo kuongeza mapato kwa TZS 288 milioni; na
(b) Ili kuepusha kurundikana sana kwa
nambari zisizotumika kwa magari yaliyokusudiwa kupitia tu nchini kwa
ajili ya biashara, kuanzisha namba maalum kwa vyombo vya moto
vinavyoingizwa kwa kusafirishwa nje ya Zanzibar kibiashara. Hatua hiyo
itaongeza mapato ya Serikali kwa TZS 347.
I. Sheria ya Kodi ya Mapato 2004 (Presumptive Tax Scheme (PTS)
67. Mheshimiwa Spika, moja ya eneo
ambalo limekuwa likilalamikiwa sana ni utaratibu wa kutoza kodi kwa
wafanyabiashara wadogowadogo katika sekta isiyo rasmi. Wengi wa
wafanyabiashara hawa hawana uwezo wa kuweka kumbukumbu zinazohitajika
kutozea kodi ya mapato na Ushuru wa Stempu. Serikali inahitaji kuwalea
wafanyabiashara hao na kuwapunguzia mzigo wa kutimiza matakwa ya
taratibu za kodi (compliance burden). Utaratibu unaotumika katika nchi
nyengine, ikiwemo Tanzania Bara, ni kuwatoza kodi wafanyabiashara kama
hawa kwa utaratibu wa “Presumptive Tax” ambao ni mwepesi zaidi kuufata
kwani unaunganisha kodi ya mapato na ushuru wa Stempu na hauhitaji
wafanyabiashara kuwasilisha Marejesho (returns) kila mwezi. Hadi sasa
utaratibu wa PTS kwa Zanzibar unatumika kwa kuwatoza kodi ya mapato
wamiliki wa magari ya biashara tu (taxi, daladala, gari za kukodisha na
za mizigo).
Inapendekezwa kutumia utaratibu huo wa
PTS kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa wafanyabiashara ambao mauzo yao kwa
mwaka hayazidi TZS 10 milioni. Wafanyabiashara wote watakaotozwa kodi
chini ya utaratibu huu hawatalazimika tena kulipa Ushuru wa Stempu.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato kwa TZS 400 milioni.
J. Marekebisho ya Misamaha ya Kodi
68. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu SMZ
imekuwa ikitumia vivutio mbalimbali ili kushajiisha uwekezaji binafsi
nchini. Moja ya sababu ya kiwango cha vivutio vilivyopo ni kasoro
mbalimbali za kisoko (market distortions) zilizokuwepo wakati huo hasa
katika kukosekana miundombinu ya msingi kama vile barabara za lami,
umeme na maji katika maeneo yote ya uwekezaji. Hivi sasa hali
imebadilika kwani tayari miundombinu hiyo inapatikana katika takriban
maeneo yote ya uwekezaji na kupelekea kupatikana mafanikio makubwa
katika uwekezaji katika sekta ya utalii hususan ujenzi wa hoteli. Haja
inayojitokeza sasa ni kupanua uwekezaji katika maeneo mengine muhimu ya
kiuchumi ambayo hayajapata msukumo mkubwa kama vile viwanda na kilimo.
Ili kuimarisha mapato ya serikali na kuweza kuvutia uwekezaji katika
maeneo mapya ya viwanda na kilimo, mambo yafuatayo yanapendekezwa:
(i) Kurekebisha Sheria ya ZIPA kwa
kufuta misamaha ya Kodi kwa vifaa vya ujenzi na vyengine vidogovidogo
kwa miradi yote ya hoteli na mikahawa. Msamaha utaendelea kutolewa kwa
vifaa vya uwekezaji (capital goods) kama vile mashine na vifaa vyengine
vikubwa vya uwekezaji;
(ii) Kuandaa na kutoa unafuu maalum kwa
uwekezaji katika viwanda, kilimo na uwekezaji wenye umuhimu maalum
(Strategic Investment) kama utakavyowekewa utaratibu hapo baadae;
(iii) Ili kuzuia udanganyifu wa thamani
ya uwekezaji unaopelekea kuonekana kiwango kikubwa cha misamaha,
kusamehe asilimia 80 tu ya mapato kwa misamaha yote ya watu binafsi,
taasisi za kidini, NGOs na uwekezaji. Kiasi kilichobakia kitakusanywa.
Hatua hizi zinatarajiwa kuiingizia Serikali jumla ya TZS 5.4 bilioni.
K. Kuimarisha Mapato kutokana na Ukodishaji wa Ardhi
69. Mheshimiwa Spika, Zanzibar ni kisiwa
kidogo na hivyo ardhi yake ni rasilimali muhimu sana. Serikali imekuwa
ikikodisha ardhi yake ili iweze kutumika kwa shughuli za uwekezaji ili
kuendeleza uchumi na jamii. Watu wengi wamekuwa wakihoji udogo wa
viwango vya kodi ya ardhi vinavyotumika Zanzibar. Pamoja na udogo wa
viwango hivyo, Serikali pia imekuwa ikisamehe kodi kwa kipindi chote cha
ujenzi wa mradi. Ili kuweza kunufaika zaidi na rasilimali hii muhimu,
inapendekezwa yafuatayo kuhusiana na kodi ya ardhi:
(i) Kuyatambua na kuyaweka katika “database” maeneo yote ya ardhi yaliyokodishwa;
(ii) Kurekebisha viwango vya kodi kwa
kuweka uwiano kwa matumizi yanayofanana kwa kuzingatia mahali lilipo
eneo na matumizi yake;
(iii) Kuweka viwango maalum vya kuvutia
uwekezaji katika maeneo ya vipaumbele vya viwanda, kilimo na miradi
maalum (strategic investments); na
(iv) Ili kuondoa mtindo wa maotoe katika
kukodi ardhi (speculation) na kuhakikisha inatumika vyema kwa maendeleo
ya uchumi, kufuta utaratibu wa kutoa muda wa msamaha kwa matumizi ya
ardhi (grace period). Anaekodishwa atalazimika kuanza kuilipia mara tu
baada ya kukodishwa.
Mwaka ujao wa fedha unatarajiwa kuwa wa
kujipanga zaidi na usimamizi ili uwezeshe kupatikana makisio sahihi ya
kodi baada ya kuimarishwa usimamizi. Hata hivyo, hatua hizi zinatarajiwa
kuiongezea Serikali mapato kwa angalau TZS 500 milioni.
L. Hatua za Kiutawala
70. Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua
zilizopendekezwa hapo juu, bado taasisi za ukusanyaji za TRA na ZRB
zitaendelea kuchukua hatua nyengine za kiutawala na utendaji zikiwemo za
kuwatambua na kuawasijili walipakodi wapya, kusimamia maeneo
yaliyoonesha udhaifu kama vile mikataba ya ukodishaji wa hoteli bila ya
kuwepo dhamana, matumizi ya “tax clearance”, kusajili Washauri wa Kodi
(Tax Consultants) na kugomboa kodi zilizo mikononi mwa walipakodi.
Inatarajiwa kuwa hatua hizi zitaongeza mapato kwa TZS 500 milioni.
Kwa jumla hatua zote zinazopendekezwa zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa TZS 16.9 bilioni.
SURA YA MAPATO KWA MWAKA UJAO WA FEDHA 2013/2014
Mapato ya Ndani
71. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka ujao
2013/14 Serikali inakusudia kuongeza juhudi ya ukusanyaji mapato yafikie
asilimia 22.1 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 21.3 ya mwaka 2012/13.
Katika mwaka ujao wa fedha, mapato kutokana na vyanzo vya ndani
yanakadiriwa kufikia TZS 324.6 bilioni. Kitaasisi, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) inakadiriwa kukusanya TZS 147.9 bilioni, Bodi ya Mapato
Zanzibar (ZRB) TZS 171.7 bilioni, TZS 5.0 bilioni gawio kutoka Benki Kuu
na Mashirika ya SMZ, TZS 26.0 bilioni zitazokusanywa na Mhasibu Mkuu wa
Serikali kama Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar na
mkopo wa ndani wa TZS 25.0 bilioni. Zikichanganywa na TZS 5.0 bilioni
za kuanzia mwaka, jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia TZS
380.6 bilioni.
72. Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2013/2014 inatarajia kupata jumla ya TZS 277.9 bilioni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha. Kati ya fedha hizo, TZS 235.4 bilioni ni kwa ajili ya Programu na Miradi ya Maendeleo ikiwemo TZS 148.6 bilioni za Mikopo na TZS 86.8 bilioni za ruzuku. Misaada ya kibajeti (GBS) inatarajiwa kufikia TZS 40.0 bilioni ikihusisha TZS 26.5 bilioni za ruzuku na TZS 13.5 bilioni ambazo ni mikopo. Kiasi kilichobakia cha TZS 2.5 bilioni kinatokana na salio la sehemu ya mgao Zanzibar kutokana na Msamaha wa Madeni (MDRI).
73. Mheshimiwa Spika, muundo wa Mapato
unaojitokeza hapo juu unamaanisha kuwa utegemezi wa bajeti kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo, unaopimwa kama uwiano wa ruzuku kwa jumla ya
matumizi, utaendelea kupungua hadi kufikia asilimia 17.2 mwaka 2013/2014
kutoka asilimia 21 mwaka 2012/2013. Aidha, uwiano wa ruzuku kwa Pato la
Taifa unatarajiwa kupungua hadi kufikia asilimia 8.5 kwa mwaka wa
2013/2014 kutoka asilimia 11.2 mwaka 2012/2013. Ni muhimu kuendelea
kuhakikisha kuwa mapato ya ndani yanakuwa kwa kasi zaidi kuliko ile ya
ruzuku.
74. Mheshimiwa Spika, mukhtasari wa
mfumo wa Bajeti ya mwaka 2013/14 baada ya hatua mbalimbali za mapato na
mgawanyo wa matumizi ni kama unavyoonekana katika Jadweli hapa chini.
Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2013/14
Maelezo Makisio Makisio Ongezeko
2012/13 2013/14 (%)
MAPATO
A. Mapato ya ndani 294.1 324.6 10.4
B. 4.5% Msaada wa kibajeti (GBS) 39.9 40.0 0.3
C. Dhamana za Hazina/Hati Fungan 15.8 25.0 58.2
D. Kodi Mapato kwa w/kazi wa SMT 0.0 26.0
E. Bakaa ya bajeti 2012/13 5.9 5.0 -15.3
F. Msamaha wa Madeni (MDRI) 2.5
G. Mikopo na Ruzuku 293.2 235.4 -19.7
Jumla ya Mapato 648.9 658.5 1.5
MATUMIZI
Matumizi ya Kawaida 307.8 353.1 14.7
i) Mishahara (Mawizara) 139.6 155.5 11.39
ii) Mishahara (ruzuku) 17.7 20.8 17.5
iii) Matumz mengineyo (Wizara) 71.1 80.6 13.3
iv) Matumizi mengineyo (ruzuku) 26.6 31.2 16.9
v) Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) 52.8 65.0 23.1
Matumizi ya Maendeleo 341.1 305.4 -10.5
i) Mchango wa Serikali 47.9 70.0 46.1
ii) Washirika wa Maendeleo 293.2 235.4 -19.7
Jumla ya Matumizi 648.9 658.5 1.5
Chanzo: Idara ya Bajeti - ORFUMM
75. Mheshimiwa Spika, sura hiyo ya
Bajeti ndiyo inayokusudiwa kutekeleza Mpango wa Maendeleo na kuendesha
kazi za kawaida kwa mwaka ujao wa Fedha. Inatarajiwa kuwa utekelezaji wa
Bajeti hiyo utupeleke karibu zaidi na kufikia malengo ya Mipango yetu
Mikuu ya Maendeleo ikiwemo Dira ya 2020, MKUZA II, Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Malengo ya Kimataifa yakiwemo Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
SHUKURANI
76. Mheshimiwa Spika, makadirio haya
yasingeweza kuwasilishwa leo hii hapa bila ya mchango wa watu na Taasisi
mbalimbali. Naomba niwashukuru wachache kwa niaba ya wengi waliochangia
mafanikio ya hatua hii muhimu. Mosi, naomba nianze kwa kumshukuru sana
Mheshimiwa Rais, ambae pia anaisimamia Ofisi yake hii ya Fedha, Uchumi
na Mipango ya Maendeleo, Makamo wa Kwanza na wa Pili wa Rais, Wajumbe
wote wa Baraza la Mapinduzi ambao ni Mawaziri na Manaibu Mawaziri wote
kwa kuipitia na kuitolea Muongozo Rasimu ya Bajeti hii. Shukrani pia kwa
Wajumbe wa Tume ya Mipango kwa kazi kubwa ya kuzingatia na kuridhia
mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha.
77. Mheshimiwa Spika, pili, naomba
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa uongozi wako mahiri na wa busara
kwa Baraza hili. Ni kwa busara, uvumilivu na uongozi wako ndio tumeweza
kuhakikisha utulivu hapa Barazani na baina ya Baraza na mihimili mingine
ya Dola. Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika. Pili, naomba nimshukuru
Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza lako,
Mheshimiwa Hamza Hassan Juma kwa mchango na muongozo wa Kamati yake.
Nawashukuru pia Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati zote za Kudumu na
Wajumbe wao kwa kukaa na Wizara zote na kupitia Mapendekezo ya Bajeti
zao na kuyatolea muongozo unaofaa. Kwa hakika, Mheshimiwa Spika,
nalishukuru sana Baraza lako lote kwa mchango wake katika maandalizi ya
Bajeti hii.
78. Mheshimiwa Spika, nje ya Baraza
Mheshimiwa Spika, naomba kuwashukuru Makatibu Wakuu na Watendaji wengine
wote wa Wizara na Taasisi zinazojitegemea, Mikoa, Manispaa na
Halmashauri za Wilaya. Nathamini na kuushukuru pia mchango wa Sekta
binafsi na Asasi zisizo za kiserikali katika maandalizi ya Bajeti hii.
Vikao vingi vimefanyika na ushauri wao umesaidia sana kufikisha Bajeti
katika muundo wake wa sasa.
79. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee
naomba kuwashukuru watendaji wa Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na
Mipango ya Maendeleo. Nawashukuru sana Katibu Mkuu ndugu Khamis Mussa
Omar, Katibu Mtendaji Bi. Amina Khamis Shaaban, na Naibu Katibu Mkuu
ndugu Juma Ameir Hafidh. Nawashukuru pia Kamishna wa Bajeti, Mhasibu
Mkuu wa Serikali, Kamishna wa Mipango ya Kitaifa, Sera za Kisekta na
Kupunguza Umaskini, Kamishna wa Ukuzaji Uchumi, Kamishna wa Fedha za Nje
na Wakuu wa Idara na Watendaji wote wa Ofisi yangu kwa kazi kubwa
waliyoifanya kwa umahiri na kujitolea hadi kufikia hatua hii.
Ninapowasilisha Mapendekezo haya leo hii nafarijika kujua kuwa
Mapendekezo haya ni matokeo ya kazi kubwa, ya umakini na ya juhudi ya
pamoja ya Wasaidizi mahiri wanaofanya kazi kwa mashirikiano makubwa na
kulitumikia Taifa letu kwa nguvu na uwezo wao wote.
80. Mheshimiwa Spika, naomba kuwashukuru
sana Washirika wetu wa Maendeleo, nchi marafiki na Mashirika ya
Kimataifa, kwa mchango wao mkubwa kwa juhudi zetu za kuwaletea maisha
bora wananchi wenzetu. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Wazanzibari wote, naomba kuzishukuru sana nchi zote zilizosaidia na
zinazoendelea kutusaidia ili nasi tupige hatua za maendeleo. Miongozi
mwa nchi hizo ni Canada, China, Cuba, Denmark, Finland, India, Ireland,
Japan, Korea, Kuwait, Marekani, Misri, Norway, Oman, Sweden, Ubelgiji,
Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu na Uturuki.
81. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Mashirika ya Kimataifa, naomba kuyashukuru sana ACBF, ACRA, AfDB, AGRA,
BADEA, CARE INTERNATIONAL, CDC, CHAI, CIDA, DANIDA, DFID, EGH, EU, EXIM
BANK ya CHINA, EXIM BANK ya KOREA, FAO, FHI, GAVI, GEF, GLOBAL FUND,
IAEA, ICAP, IDB, IFAD, ILO, IMW, IPEC, JICA, JSDF, KOICA, KUWAITI FUND,
MCC, NORAD, OFID, ORIO-Netherlands, PRAP, SAUDI FUND, SAVE THE CHILDREN,
SIDA, UN AIDS, UNDP, UNESCO, UNFPA, UN-HABITAT, UNICEF, UNIDO, USAID,
WB, WHO, WSPA.
82. Mheshimiwa Spika, mwisho, na kwa
namna maalum, naomba kwa dhati kabisa kuwashukuru sana Wananchi wote wa
Zanzibar kwa imani yao kwa serikali na Watendaji wake na Baraza lako
hili. Bila ya imani ya Wananchi, leo hii kazi zetu zingeweza kufanyika,
bila ya utulivu wao sote tusingeweza kuwa makini na bila ya ridhaa yao,
sote tusingekuwepo. Kwa mara nyengine tena, nawaomba Wananchi wote
waendelee kushirikiana nasi waliotutuma kuwatumikia ili kwa pamoja
tuweze kuleta maendeleo ya nchi yetu na sisi wenyewe na kizazi chetu.
HITIMISHO
83. Mheshimiwa Spika, tunaendelea kupata
mafanikio katika ukuzaji wa uchumi wetu na uimarishaji wa huduma
mbalimbali za jamii. Hata hivyo, lazima tubaini kuwa kazi iliyo mbele
yetu ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu na jamii yake ni kubwa sana.
Tunahitaji kujituma kwa jitihada na maarifa zaidi, sote kwa pamoja,
serikalini na sekta binafsi.
84. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo
hayo, sasa naomba kwa heshima na taadhima, Baraza lako tukufu lipokee,
kujadili na hatimae kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na
Bajeti kwa mwaka 2013/14 kwa kuzingatia Mwelekeo wa Hali ya Uchumi. Kama
nilivyosema, Bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni Bajeti ya Huduma za Jamii
kwa Wananchi wa Zanzibar. Serikali inapendekeza mbele ya Baraza lako
tukufu kukusanya mapato ya Shilingi mia sita na hamsini na nane bilioni
na mia tano milioni (TZS 658.5 bilioni). Serikali pia inapendekeza
kutumia kiasi hicho cha Shilingi mia sita na hamsini na nane bilioni na
mia tano milioni (TZS 658.5 bilioni) ikiwemo Shilingi mia tatu na
hamsini bilioni na mia moja milioni (TZS 353.1 bilioni) kwa kazi za
kawaida na Shilingi mia tatu na tano bilioni na mia nne milioni (TZS
305.4 bilioni) kwa kazi za maendeleo.
85. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
JUNE 12, 2013
Source: Zanzi News
No comments:
Post a Comment