ASEMA SMG, BASTOLA ZILITUMIKA ARUSHA
MWENYEKITI
wa CHADEMA Freeman Mbowe, amevituhumu vyombo vya dola kuwa vinawafahamu
watu walioshiriki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea juzi katika viwanja
vya Soweto kwenye mkutano wa chama hicho.
Mbowe,
alisema tukio hilo ni la kupangwa na wamegundua risasi za bunduki aina
ya SMG na bastola zilitumika mara baada ya mlipuko huo jambo linalozusha
hofu na kudidimiza demokrasia ya vyama vingi.
Wakati Mbowe
akitoa tuhuma hizo kwa vyombo vya dola, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),
Said Mwema ameunda timu itakayoongozwa na makamishna wawili (Paul
Chagonja na Isaya Mungulu), kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu ya
uchunguzi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mkoani hapa, Mbowe alisema uchunguzi wa
awali walioufanya wamebaini tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Alisema ni
vema serikali ikatangaza kuachana na mfumo wa vyama vingi kuliko
kuruhusu mauaji na vurugu katika mikutano ya vyama vya upinzani
vinavyoonekana kutoa wakati mgumu kwa watawala.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa awali katika eneo la tukio umebaini bomu lililolipuliwa ni la kiwandani na si la kutengenezwa.
Mbowe
alisema risasi hizo pia ni miongoni mwa zilizopigwa kwenye tanki la
mafuta la gari la matangazo la CHADEMA ambapo zililitoboa.
Alibainisha kuwa inavyoonekana wahusika walitaka kuzalisha mlipuko mwingine mkubwa na kuleta maafa makubwa katika mkutano huo.
“Haihitaji
uchunguzi wa kwenda mwezini katika suala hili, ni wazi walipanga kutuua
lakini wakaua watu wasiohusika. Waliouawa hawakuwa katika mpango wao na
wamekuwa wahanga kwa niaba yetu.
“Hata kama
utaamua kumuua Mbowe au (Godbless) Lema, huwezi kuiua CHADEMA kwani
chama kitabaki, na wanachama wengine wataendeleza harakati za chama kama
kawaida,” alisema.
Wabunge kutohudhuria Bunge
Mbowe
alisema kutokana na tukio hilo ambalo limeua watu zaidi ya watatu,
CHADEMA imeamua kulifanya ni la kitaifa na wabunge wake watashiriki
kwenye maombolezo.
Alisema
kuanzia leo wabunge wote wa CHADEMA hawatahudhuria vikao vya Bunge na
watajumuika mkoani Arusha hadi misiba yote itakapomalizika.
Alisema
wanatarajia kufunga mahema katika eneo la tukio na marehemu wote
wataagwa katika eneo hilo ambapo ibada zote za Kiislamu na Kikristu
zitafanyikia hapo.
IGP aunda timu
Mkuu wa
Jeshi la Polisi (IGP), Mwema ameunda timu ya kuongeza nguvu ya uchunguzi
itakayoongozwa na makamishna wawili ambao ni Paul Chagonja kutoka idara
ya operesheni na Isaya Mngulu kutoka ofisi ya upelelezi makao makuu.
IGP Mwema
alisema baada ya tukio hilo, jeshi hilo lilituma makamishna wawili
kutoka makao makuu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio
hilo na kwamba wameshaanza kukusanya taarifa mbalimbali zitakazoweza
kusaidia kuwabaini watu waliohusika.
Alisema
wameunganisha nguvu na vyombo vingine vya ulinzi na watawasaka wahalifu
hao pamoja na walio nyuma yao kwa kile alichoeleza tukio hilo
linaashiria kushamiri kwa matendo ya kigaidi nchini.
Akizungumzia
tuhuma zinazotolewa na wananchi juu ya Jeshi la Polisi kuwajeruhi watu
kwa risasi za moto, IGP Mwema alisema kila taarifa inafanyiwa kazi kwa
umakini na kwamba baada ya uchunguzi watatoa taarifa kamili kwa umma juu
ya kilichotokea jijini Arusha.
Aliwaomba
wananchi wenye taarifa za kuweza kumtambua aliyerusha bomu pamoja na
watu walio nyuma yake wajitokeze au wamtumie ujumbe kupitia simu yake ya
mkononi namba 0754 78 55 57 na kwamba uhusika wao utafanywa kuwa siri.
IGP Mwema
pia alisema watachunguza kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) bara, Mwigulu Nchemba aliyowaambia wakazi wa Kimandolu
kuwa wasipoichagua CCM katika uchaguzi wa madiwani wa Jiji la Arusha
ulioahirishwa jana, watakufa.
Mwema
alisema watachunguza kauli hiyo baada ya kuulizwa swali la hatua
zilichochukuliwa kabla na baada ya mlipuko huo dhidi ya kauli ya
Nchemba.
Juzi katika
mkutano wa kufunga kampeni za udiwani kwa CHADEMA uliofanyika kwenye
viwanja vya Soweto, kitu kinachodhaniwa ni bomu kilipuka na kuua watu
watatu na wengine kujeruhiwa.
SOURCE: CHADEMA SOCIAL MEDIA
No comments:
Post a Comment