MAKUNDI YA URAIS YACHOCHEA MAANDAMANO KUPINGA SERIKALI TATU
CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM), kimeweka mkakati wa kuipinga rasimu ya Katiba mpya,
hususan pendekezo la muundo wa serikali tatu, Tanzania Daima Jumapili
limebaini.
Mkakati huo
umekuja baada ya kubaini kuwa rasimu ya Katiba mpya iliyopendekeza
muundo huo imekipasua chama hicho katika makundi yanayohatarisha uhai wa
chama.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na mawaziri, wabunge, viongozi
na makada mbalimbali wa chama hicho tawala, umebaini kuwa makada wengi
wameshangazwa na hatua ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Warioba kuruhusu
pendekezo la kutaka muundo wa serikali tatu liingizwe kwenye rasimu.
Tayari
Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
ambaye anatajwa kutaka kuwania urais amepinga pendekezo hilo, kwa madai
kwamba hakuna nchi inayoongozwa na marais watatu duniani.
Makundi mengine ya urais yanadai kuwa rasimu hiyo ikipita itawaweka njia panda wasijue wagombee nafasi gani ifikapo mwaka 2015.
Baadhi ya
vigogo wa chama hicho waliliambia gazeti hili kuwa lawama za kwanza
wanazielekeza kwa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwa
madai kuwa aliiona rasimu hiyo kabla ya mtu mwingine yeyote na kuiacha
kamati ya Jaji Warioba ikija na pendekezo la kutaka serikali tatu.
“Kwanza
Ilani yetu inazungumzia serikali mbili, kule Zanzibar Rais Ali Mohamed
Shein na Naibu Katibu Mkuu Visiwani wanagombana na Wazanzibari wa CUF
kila siku kuhubiri serikali mbili, leo rasimu inakuja na serikali tatu
na rais anaiona na anaipitisha ije kwa wananchi. Hatumuelewi,” alisema
mmoja wa viongozi wa chama hicho, mjumbe wa NEC kutoka mikoa ya Kanda ya
Ziwa.
Kigogo huyo
alisema chama kinasubiri kwa hamu kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC),
inayotarajiwa kukutana Jumatatu ijayo jijini Dar es Salaam, maalumu kwa
ajili ya kujadili rasimu hiyo ya Katiba na kutoka na msimamo wa chama.
Kada
mwingine ambaye ni mwenyekiti wa CCM kwenye moja ya mikoa ya Kanda ya
Kati, alilieleza gazeti hili kuwa kilichotokea ndani ya chama hicho
kuhusu pendekezo la serikali tatu ni kama bomu lililolipuka ghafla.
“Mimi
nakuambia kilichotokea ni kama bomu vile, sasa kila mtu amenyanyuka,
anakung’uta vumbi na kuanza kuvuta fikra nini kimetokea. Nadhani kikao
cha CC kesho kutwa ni muhimu sana na lazima tuwe na NEC kabla ya Bunge
kumalizika tukawekane sawa,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM mkoa.
Kabla ya
chama hicho kuitisha kikao cha CC ya dharura, baadhi ya makundi ya urais
yalielezwa kuanza kupanga njama na mikakati ya kuwachonganisha baadhi
ya wafuasi wao kuitisha maandamano kupinga pendekezo la serikali tatu.
Mikakati ya kuzima serikali tatu
Wakati Wana
CCM wengi wamegawanyika kutokana na rasimu ya pendekezo hilo, upande wa
pili wanajipa moyo kwamba hoja hiyo haitapita kuwa sheria ndani ya
Katiba mpya.
Moja ya
mikakati inayofanywa na chama hicho kwa sasa ni kuhakikisha nakala ya
rasimu hiyo inawafikia wanachama ngazi ya tawi ili wailewe na kuwataka
wawe makini wakati wa upigaji kura kupinga baadhi ya mambo wasiyoyataka,
ikiwamo hoja ya kutaka kuwa na serikali tatu.
Pia chama
hicho kimeanzisha mabaraza ya Katiba ya chama ili kuwapa fursa zaidi
wanachama wao kuijua rasimu hiyo na kushiriki kikamilifu kuipitisha.
Wabunge Viti Maalumu wacharuka
Baadhi ya
wabunge wa Viti Maalumu waliliambia gazeti hili kuwa pendekezo hilo
linaonesha wivu wa wajumbe wa tume hiyo kwa wabunge hao.
“Umoja wa
wanawake (UWT) ulishapitisha azimio kwamba ukomo wa Viti Maalumu ni
awamu mbili. Lakini kusema viti hivyo viondoke, havina maana, ni uamuzi
uliotokana na wivu,” alisema mbunge mmoja wa Viti Maalumu ambaye aliomba
jina lake lihifadhiwe.
Mbunge huyo ambaye aliungwa mkono na wenzake, alisema watahakikisha hoja hiyo haipiti na kuingizwa kwenye Katiba mpya.
Wiki
iliyopita, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa rasimu ya mapendekezo ya
katiba mpya ambayo imesheheni masuala mazito ambayo kama yatapitishwa
yataleta mabadiliko makubwa ambayo yamekuwa yakipiganiwa kwa zaidi ya
miaka 20.
Miongoni mwa
mambo makuu yaliyoingizwa katika rasimu hiyo ni mfumo mpya wa Muungano
wa serikali tatu; serikali ndogo ya mawaziri 15; Tume Huru ya Uchaguzi;
spika na naibu wake wasio wabunge wala viongozi wa vyama vya siasa.
Mengine
yaliyoingizwa ni kumnyang’anya rais madaraka ya kuteua peke yake
viongozi wa ngazi za juu. Tume inapendekeza kwamba rais adhibitiwe
katika kuteua mawaziri na manaibu wao, majaji na manaibu wao, wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama na makatibu wakuu na manaibu wao.
Imependekeza
rais asaidiwe na vyombo kadhaa katika uteuzi huo. Mawaziri
watakaoteuliwa na rais hawatashika nyadhifa zao hadi waidhinishwe na
Bunge. Vile vile, rais atateua majaji kutoka miongoni mwa majina
yatakayopendekezwa kwake na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tume
imependekeza liundwe Baraza la Ulinzi na Usalama litakalomshauri rais
kuhusu uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Zaidi ya
hayo, kinga ya rais kutoshitakiwa imependekezwa ibaki pale pale, ingawa
Bunge lina mamlaka ya kumshitaki kama ilivyo sasa.
Rasimu pia
imependekeza umri wa mgombea urais ubaki miaka 40 ya sasa. Katika
uchaguzi, rais atatangazwa mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya
asilimia 50 ya kura zote; na matokeo yake yatahojiwa mahakamani ndani ya
mwezi mmoja tangu yalipotangazwa.
Mbali na
kurejeshwa kwa taifa la Tanganyika, tume imependekeza pia mgombea
binafsi aruhusiwe katika ngazi zote, kuanzia kitongoji hadi Ikulu.
Akisisitiza
umakini uliotumika kuchakata mapendekezo yaliyokusanywa kwa wananchi
tangu Aprili mwaka jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Warioba alisema
wamezingatia masilahi ya taifa na mahitaji ya wakati katika kila eneo.
Source: Chadema Social Media
No comments:
Post a Comment